Serikali ya India imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha lengo la utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 linafikiwa, hatua itakayosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
Hayo yamebainika wakati wa kikao kati ya Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme na Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Juni 20, 2024.
Katika mazungumzo hayo, Bi. Mndeme ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa huduma za maendeleo ya kijamiii na kiuchumi kwa wananchi.
Mndeme ameeleza kuwa ajenda ya nishati safi ya kupikia ni moja ya kipaumbele cha kimkakati cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara katika kuhamasisha jamii na juhudi zake zinashuhudiwa na Watanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
“Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ametumia ushawishi wake katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa kutafuta fursa ili kubadilisha mfumo uliopo katika jamii yetu kwa kuacha kutumia nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia kama gesi” amesema Mndeme.
Aidha Mndeme amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira linaendelea kupewa kipaumbele katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya ngazi za maamuzi.
Mndeme pia ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kutoa fursa ya mafunzo yanayolenga katika kuwajengea uwezo kwa wataalamu kada mbalimbali ikiwemo sekta ya mazingira.
Kwa upande wake, Balozi Mhe. Verma amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha jamii yake inahamia katika mfumo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia hatua inayolenga kuepukana na matumizi ya nishati chafu ambayo imekuwa na madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira.
“India imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo takribani asilimia 80 ya wananchi wa mijini na vijijini wanatumia nishati hiyo…..Tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha ajenda hii inafikiwa kwa wananchi wake” amesema Mhe. Verma.
Aidha Mhe. Verma ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni moja ya ajenda inayoendelea kupewa kipaumbele katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya kikanda, kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu kugusa maslahi ya wananchi wengi hususani waliopo katika mataifa yanayoendelea.
Mhe. Verma amefafanua kuwa umuhimu huo unatokana na ukweli kuwa Tanzania na India ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea ambayo yamekuwa yakikabiliana kwa vitendo na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo moja ya juhudi hizo pamoja na kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo imekuwa tegemezi kwa jamii nyingi za maeneo ya vijijini.
Ameongeza kuwa katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, tarehe 5 Juni mwaka huu Serikali ya India imezindua Kampeni ya Upandaji Miti ijulikanayo “A tree for Mother” inayolenga kuhamasisha dunia umuhimu wa kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na rasilimali za viumbe hai mbalimbali.
Hivyo, Balozi Verma ameiomba Serikali ya Tanzania kuunga mkono kampeni hiyo, ambapo katika kipindi cha mwaka 1 Serikali ya India imekusudia kupanda miti bilioni 1 hatua inayolenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda mazingira na uhifadhi wa baianoai mbalimbali na hivyo kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Deogratius Paul na watalaamu mbalimbali