Taasisi ya Blue Carbon UAE na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametia saini Mkataba wa Makubaliano kuanza kwa ushirikiano wenye lengo la kukuza usimamizi endelevu wa misitu na kupunguza ukame.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe, Dkt. Selemani Jafo amesema biashara ya kaboni itasaidia kuleta fursa nyingi hapa nchini na kusaidia kuhifadhi mazingira.
Amesema hayo mara baada ya hafla ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya uhusiano kati ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Kampuni ya Blue Carbon kutoka Dubai.
Hafla hiyo imeshuhudiwa na Mwanamfalme wa Dubai ambaye pia ni Mwenyekiti wa kampuni ya Blue Carbon Mhe. Sheikh Ahmed Dalmook Al Maktoum na Waziri Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.
Dkt. Jafo amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa makubaliano hayo baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kukamilisha uandaaji wa kanuni na mwongozo wa biashara ya kabini Oktoba 2022.
Amesema hatua ya kusainiwa kwa makubaliano hayo itafungua milango kwa wananchi kupanda miti kwa wingi na kutunza mazingira ili iweze kuingia kwenye biashara hiyo.
“Ni Imani yetu sasa tutategemea kuwa na fursa nyingi pamoja na kurudisha hali ya mazingira iliyoharibika na tunaona hata mikoko pia inaingia katika baishara ya kaboni hivyo TFS sasa watakuwa na uwanja mpana wa kuhakikisha misitu yetu inahifadhiwa,” amesema.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo Mwanamfalme Mhe. Sheikh Al Maktoum ambaye aliambatana na ujumbe wake Ushirikiano huo utajikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi, kusimamia na kusajili rasilimali zake za misitu.
Amesema hifadhi hizo zenye ukubwa wa hekta milioni 8 katika awamu ya kwanza ya kwanza ikijumuisha hekta 56,000 za mikoko chini ya kifungu cha 6 cha Mkataba wa Paris hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, katika kuendeleza miradi mipya ya kukabiliana na kaboni.
“Tuna heshima kubwa kusaini Mkataba huu na Serikali ya Tanzania. Ushirikiano huu unawakilisha hatua muhimu katika kukuza mazoea ya usimamizi endelevu wa misitu na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.”
Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kuhifadhi rasilimali za misitu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, na ushirikiano huu na Blue Carbon utasaidia kufikia malengo hayo. Ushirikiano huo pia utatoa fursa kwa jumuiya za wenyeji kushiriki katika miradi ya kukabiliana na kaboni, na hivyo kukuza ukuaji endelevu wa uchumi na kuboresha maisha.
Kwa upande wake Waziri Dkt. Pindi ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapanda mit kwa wingi hasa katika kipindi hiki cha mvua ili iweze kukua na kuingia katika biashara ya kaboni.
Amesema kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo la takriban hekta milioni 48.1 zenye misitu ambayo imekuwa na faida nyingi kwa wananchi wake katika masisha ya kila siku.
“Tukitunza misitu yetu tutapata faida nyingi kwan tunaona vyanzo vya maji vinategemea misitu, sekta nyingi zinategemea miti mfano kilimo, afya, ujenzi, mindombinu hivyo ni kuhimu kulinda kuhifadhi misitu,” amesisitiza.
Naye Kamishna wa Uhifadhi TFS Prof. Dos Santos Silayo amesema wakati umefika sasa kwa nchi zilizoendelea kuweka mchango wao kwa nchi zinazoendelea kupunguza gesi joto.
Amesema hatua ya kusaini makubaliano na Blue Carobon ni mwanzo wa utekelzaji wa shughuli hizi ambapo kampuni hiyo itaanza mchakato wa kusajili kuzingatia maelekezo.
Ametoa msukumo kwa nchi zinazoendelea kuweka kipaumbelea katika kuhifadhi mistu ili kuweka msingi wa maeneo yanayoweza kujikita katika biashara ya kaboni ambayo imeshakuwa ni mbadala wa shughuli za kiuchumi hivi sasa.