Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo ameielekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA) kuweka utaratibu wa kuhakikisha ujenzi wa barabara unaenda sambamba na upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Pia ,amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaenda sambamba na suala zima la usafi kwa kuweka maeneo ya viwanda na kampuni katika hali ya usafi.
Dkt.Jafo ametoa maelekezo hayo leo tarehe 01 Juni,2024, jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kampeni ya Usafi wa Mazingira Kitaifa ambapo kwa Dodoma imefanyika eneo la Mailimbili.
“Najua tuna ujenzi wa barabara ya mzunguko hapa Jiji la Dodoma zaidi ya Kilomita 112 katika eneo hili bado hali haijaridhisha,wenzetu wanaojenga barabara wanahamisha goli,nikiwa Waziri wenye dhamana nielekeze TANROADS na TARURA,wanapojenga barabara ni lazima wasimamie ajenda ya upandaji wa miti,hatuwezi kutumia fedha nyingi halafu tunamaliza barabara unaona haijajali mazingira,hapana,”amesema Waziri Jafo.
Aidha, Waziri Jafo amezielekeza Manispaa na Majiji yote Nchini kuweka vifaa ya kuhifadhia taka kwenye maeneo yao ikiwa ni utekelezaji wa Kampeni ya My Dustbin.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema wataendeleo kutimiza azma ya serikali ya kulifanya Jiji la Dodoma kuwa safi wakati wote kwa kuendelea kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi.
Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira mwaka huu yameanza tarehe 27 Mei na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 05 Juni yakichagizwa na kauli mbiu isemayo Urejeshwaji wa ardhi,ustahmilivu wa hali ya Jangwa na Ukame ambapo kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.