Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema taasisi mbalimbali zimetekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hadi kufikia wiki hii, vyuo 30 kati ya 35 vilivyopo hapa nchini vimeanza kutekeleza maelekezo hayo kwa kuanza kutumia nishati mbadala.
Pia, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Magereza limeonesha utayari wa kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni hatua ya kupunguza ukataji wa miti ambao ni chanzi cha uharibifu wa mazingira.
Mhe. Khamis amesema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021 – 2026) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Oktoba 24, 2023.
Amebainisha kuwa maelekezo hayo ya Serikali hayahusu mwananchi mmoja mmoja bali yanazilenga taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 ambazo zina matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Mhe. Khamis amesema kuwa katazo la matumizi ya kuni na mkaa limelenga kuhifadhi mazingira na kwamba linatokana na maazimio ya Kamati ya Kitaifa ya Nishati Salama ambapo kila taasisi ilipewa majukumu ya kutekeleza.
Akiendelea kutoa ufafanuzi mbele ya Kamati ya Bunge Naibu Waziri amesema Serikali inatekeleza katazo la kuni na mkaa na kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti.
“Kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa baadhi ya taasisi za Serikali kwa mfano Shule ya Wasichana Ruvu imeacha kabisa matumizi ya kuni na mkaa na wamesave (wameokoa) fedha zaidi ya asilimia 50 hadi 60,” amesema.
Aidha, Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na kampuni za gesi zikiwemo Taifa na Oryx ambazo zimeonesha utayari wa kushiriki katika kampeni hiyo ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuingia katika nishati safi ya kupikia.
Kuhusu Mkakati wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021 – 2026), Naibu Waziri Khamis amesema una lengo la kujenga uwezo wa kitaifa wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwezesha nchi kutumia njia zenye uzalishaji mdogo wa gesijoto katika kufikia maendeleo endelevu.
Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imeandaliwa Dira na Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii yote ya Watanzania kwa lengo la kunusuru mazingira yasiharibike.