Sima apiga marufuku uokotaji wa chupa dampo

Aug, 12 2020

Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeagizwa kuanzisha programu maalumu ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya utenganishaji wa taka kuanzia ngazi ya kaya ili kutofautisha aina ya taka za kurejeleza na zile za kupeleka dampo.

Agizo hilo limetolewa hii leo Mkoani Mbeya na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima wakati wa ziara ya kikazi katika dampo la Nsagala lenye ukubwa wa hekta 28 na kumuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Amede Ng’wanidako kushirikiana na Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya kina ya kuboresha dampo hilo.

Amesema ujenzi wa huo wa dampo la kisasa utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zitakazolishwa katika Jiji la Mbeya zitapelekwa dampo kwa wakati na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

“Huwezi kutenganisha afya na mazingira, mradi huu ni mkubwa sana na kwa namna utakavyotekelezwa hatutaraji kuona taka mjini zinazagaa.Tunatarajia kuona taka zote zinakuja hapa zikiwa zimetenganishwa” alisema Naibu Waziri Sima.

Akiwa katika eneo hilo la dampo la Nsagala, Mhe Sima ameshuhudia wananchi wakiingia kiholela katika dampo hilo kwa ajili ya kuokota bidhaa mfano chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.

“Serikali inatumia pesa nyingi katika huduma za afya ni wakati sasa tupunguze mzigo huu kwa magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mazingira safi na salama. Kuanzia sasa ni marufuku wananchi kuingia dampo kuokota chupa za plastiki, hii inahatarisha afya zao wenyewe, hivyo utaratibu wa kutenganisha taka uanzie katika vyanzo vya uzalishaji” Sima alisisitiza.

Awali Mwenyekiti wa Bodi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Esnat Chaggu amesema kwa hali ilivyosasa katika dampo hilo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa upo uwezekano wa dampo hilo kujaa mapema.

“Inabidi ufanyike utafiti wa kina zaidi kuhusu hili dampo, kwakuwa taka zote zinazozalishwa majumbani zinaletwa hapa bila kutenganishwa hivyo afya za watu ziko hatarini hususan hawa wananchi wanaokuja kuokota taka hizi hapa dampo” alisisitiza Prof. Chaggu.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka amesema kuwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 119 kinazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutafuta namna bora ya kuteketeza taka ngumu katika maeneo yao na kuainisha jitahada za pamoja zinahitajika katika kutoa elimu kwa jamii kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Kata.

Amesema NEMC iko tayari kushirikiana na Jiji katika utoaji wa elimu katika ngazi zote na kusisitiza mpango kazi huo kutekelezwa mara moja.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Bw. Vanika Ndelekwa amemuhakikishia Naibu Waziri uzingatiaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na utekelezaji wake kuanza mapema wiki ijayo. Dampo la Nsagala lina vitalu (cells) tatu za kuhifadhi taka ngumu na lina uwezo wa kuhudumia taka za Jiji kwa kipindi cha miaka 18

Naibu Waziri Mussa Sima, yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuzipatia ufumbuzi changamoto za kimazingira, kukagua uzingatia wa sheria ya Mazingira katika maeneo ya migodi na sehemu za kuteketeza taka pia kujiridhisha endapo utaratibu wa kutenganisha taka unazingatiwa ili kuzuia wananchi kuzifuata dampo hususan bidhaa zinazo rejelezeka.

Settings