​Siku ya Mazingira Duniani inatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hifadhi ya mazingira - Jafo

May, 18 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, amesema kuwa maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yanatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali ya umuhimu wa Hifadhi ya mazingira katika Nchi kwa kuelimisha wananchi na kushirikiana katika shughuli za Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa kutumia mbinu mbalimbali katika kukabiliana Mabadiliko ya Tabianchi.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jijini Dar es Salaam. Amesema kama inavyofahamika kila mwakatarehe 5 Juni, Tanzania inaungana na Nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani, hivyo kwa mwaka huu maadhimisho hayo Kitaifa yatafanyika jijiniDodoma ambapo wananchi watahamasishwa kupanda miti, kufanya usafi na kuelekezwa njia sahihi ya kutenganisha taka kwa lengo la kurahisisha utupaji wa taka, kubaini fursa zilizopo katika urejelezaji wa taka na kutumia nishati ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Waziri Jafo amesema kuwa katika maadhimisho hayo kutakua na maonyesho, zoezi la upandaji miti na matembezi ya hiyari yatakayofanyikatarehe 29 Mei, 2021 na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye ataungana na wananchi wa jiji la Dodoma, Wabunge na viongozi mbalimbali wa Serikali katika matembezi hayo kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali.

Waziri Jafo amebaiisha kuwa katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na warsha ya mafunzo kwa maafisa Mazingira wa Mikoa, Halmashauri na Wilaya zote nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika kutekeleza majukumu katika maeneo wanayosimamia.

Vile vile Mhe. Jafo amesema kuwa katika kilele cha siku ya Mazingira Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango atazindua kampeni kabambe ya Kitaifa ya uhifadhi na usafi wa mazingira yenye lengo la kuongeza kiwango cha ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali katika kuhifadhi mazingira ili kulinusuru Taifa na majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira.

Akitoa ufafanuzi Mhe. Jafo amesema kuwa katika kuhifadhi mazingira kila mmoja ana wajibu kwa nafasi yake na kutoa rai kwa vyombo vya habari tuelimishe jamii namna ya kuhifadhi mazingira kuepuka majanga mbalimbali yanayotokana na uharibifu wa mazingira

"Natoa wito kwa Mikoa yote kutumia Radio za Halmashauri za Mikoa yetu kuhamasisha na kuelimisha jamii masuala ya hifadhi ya mazingira ikiwemo kutumia nishati mbadala wa mkaa majiko banifu pamoja na kutumia njia sahihi za kuhifadhi taka" amesema Mhe.Jafo

Katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Serikali inafanya juhudi mbalimbali ili kuhifadhi mazingira kwa Maendeleo Endelevu. Kaulimbiu ya Kitaifa ya maadhimisho kwa mwaka huu ni " Tutumie Nishati Mbadala: kuongoa mfumo ikolojia".

Settings