Serikali yawataka wenye viwanda kujenga mifumo ya kudhibiti majitaka

Sep, 18 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande amewataka wenye viwanda kote nchini kujenga mifumo thabiti ya kudhibiti majitaka yasitiririke kwenye makazi ya watu.

Chande amesema hayo alipotembelea na kukagua hali ya mazingira katika viwanda vya Tanzania Breweries Limited (TBL), Raha Bevarage, Fiber Board na bwawa la majitaka la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) vilivyopo jijini Arusha.

Akizungumza katika ziara hiyo alisema ameridhishwa na namna wanavyochakata majitaka na mfumo mzima wa majitaka katika viwanda hivyo hatua inayosaidia kuepusha uchafuzi wa mazingira na maradhi na kuwataka wengine kuiga mfano huo.

Chande akiwa ameambatana na wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini alionesha kuridhishwa na mifumo ya kudhibiti majitaka wa viwanda hivyo inayosaidia kuyachakata na kutumika tena kwa shughuli mbalimbali viwandani hapo.

“Lengo la ziara hii ni kuangalia namna gani Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake mazingira inavyotekelezwa, nchi yetu inahitaji sana uwekezaji wa viwanda lakini ni lazima vizingatie utunzaji wa mazingira,” alisema Chande.

Hata hivyo Naibu Waziri Chande alisema kuwa vipo baadhi ya viwanda nchini ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi kutokuwa na mifumo bora ya majitaka hivyo kutiririka ovyo katika makazi ya watu wakidai hayana madhara hivyo Serikali itapeleka wataalamu wake kujiridhisha.

Kwa upande wake Meneja wa TBL Arusha, Bw. Joseph Mwaikasu alisema katika kiwanda hicho majitaka yanayozalishwa yanachakatwa na kutumika tena katika shughuli za mbalimbali kiwandani hapo bila kuathiri jamii.

Aidha, Mwaikasu aliongeza kuwa pia wanashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa zikiwemo na Mamlaka ya Bonde la Pangani katika kutunza maji.

Akiwa katika kiwanda cha Fiber Board aliutaka uongozi kutumia nishati mbadala wa kuni ambazo hutumika katika uzalisha wa bidhaa zake na kuondokana na kuni ambazo huchangia ukataji miti kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na kuridhishwa na mradi wa kutibu majitaka eneo la Terati aliitaka AUWSA inayoendesha mradi huo kuharakisha ufungwaji wa vifaa katika maabara ili kujirisha kuhusu usalama wa maji hayo.

Hivyo alisema kuwa maabara hiyo ikikamilika itakuwa msaada mkubwa hata kwa taasisi zingine zenye uhitaji wa kupima majitaka.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Gasto Mkawe alisema Maabara imeshajjemgwa na imekamilika na ndani ya wiki mbili vifaa vitakuwa vimefika.

Mhandisi Mkawe aliongeza kuwa ili kazi ya upimaji ianze ni lazima mabwawa yaje maji na ndani ya miezi miwili yakuwa yamejaa na hivyo kuwezesha kazi ya upimaji kufanyika.

Settings