Serikali imetoa wito kwa wadau wote kuunga mkono katika kuhakikisha agenda ya Kupunguza, Kutumia Tena na Kurejeleza Taka inakuwa ni ya kipaumbele ili kuyatunza na kuyalinda mazingira.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi, 2025.
Amewasihi wadau wakiwemo wazalishaji wa nguo, wasambazaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kushiriki katika juhudi hizi za kuwezesha taka sifuri kwenye sekta ya nguo.
Mhe. Khamis amefafanua kuwa taka ni fursa ya kiuchumi, kwani uwekezaji katika kuchakata nguo unaweza kutoa ajira nyingi na kuongeza thamani katika sekta ya viwanda.
Aidha, amesema uzalishaji wa taka umekuwa changamoto kubwa duniani kote, hususan katika miji mikubwa ambapo wastani wa asilimia 45 hadi 50 tu hukusanywa na kutupwa dampo huku asilimia 50 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mito na mifereji ya maji taka na mitaro ya maji ya mvua.
Kutokana na changamoto hizo, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti taka kwa kutumia dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu.
Naibu Waziri Khamis ameongeza kuwa Serikali inahamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za kuchakata taka, uwekezaji katika viwanda vya urejelezaji na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha taka zinapunguzwa, zinatumika tena na zinachakatwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Semesi amesema Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka Duniani ilianzishwa ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu athari za taka kwa mazingira na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali.
Amesema siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Machi ili kuhamasisha Serikali, Sekta binafsi na jamii kwa ujumla kubadili mifumo ya uzalishaji na matumizi ili kufikia uchumi wa mzunguko na mazingira safi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ameyataja malengo ya siku hii kuwa ni kuhimiza kupunguza uzalishaji wa taka (reduce), kutumia tena bidhaa (re-use), na kuchakata taka (recycle) yenye kuleta tija katika matumizi bora ya rasilimali zetu ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Kuwezesha Taka Sifuri kwenye Sekta ya Nguo na Mitindo" ikiwa na lengo la kuhimiza matumizi endelevu ya bidhaa za nguo na kupunguza taka zitokanazo na sekta hii.
Kwa upande wa Tanzania, kaulimbiu ni "Taka ni Fursa" ikisisitiza kuwa taka si uchafu bali ni malighafi yenye thamani, endapo itasimamiwa vyema.