Serikali imetoa wito kwa wananchi kushikamana na kuchukua hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti katika maeneo waliyopo.
Wito huo umetolewa leo Novemba 04, 2024 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis.
Mhe. Pinda amewataka wabunge kuunga mkono juhudi za Serikali katika kunusuru mazingira yakiwemo ya pwani ambayo yanaathiriwa na maji ya bahari na kuingia kwenye makazi ya wananchi.
“Niwaombe wabunge tushikamane nchi nzima tupande miti kwa mfano mikoko ambayo haiharibiki bila kuharibiwa, tunamuona Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan) anavyopambana kulinda mazingira na pia Makamu wetu wa Rais (Mhe. Dkt. Philip Mpango) ambaye amepewa dhamana ya mazingira anavyofanya kazi hivyo, nasi tuungane na Serikali yetu katika kulinda na kuboresha mazingira yasiharibike kutokana na shughuli za kibinadamu,” amesisitiza Mhe. Pinda.
Awali akijini swali la msingi la Mbunge wa Chakechake Mhe. Ramadhani Suleiman Ramadhan lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Mtoni Mhe. Abdulhafar Idrisa Juma aliyetaka kujua ni lini Serikali itafanya tathmini ya athari za kimazingira zilizosababishwa na maji bahari kwenye mashamba ya mpunga katika Bonde la Tibirinzi Chakechake.
Akijibu swali hilo, Mhe. Pinda amesema mwaka 2013, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilifanya tathmini ya mazingira katika eneo la Tibirinzi ambapo matokeo ya tathmini hiyo yalibainisha kuwa jumla ya hekta tano zimeathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, SJMT kwa kushirikiana na SMZ imepanga kukusanya taarifa za kina zitakazowezesha kubaini athari za kimazingira na kijamii katika maeneo yanayovamiwa na maji ya bahari ikiwemo eneo hilo ili kubaini viwango vya athari na hatua za kuchukua katika kukabiliana nazo.
Wakati huo, Naibu Waziri Pinda amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yaliyoathirika na maji ya bahari kisha itaangalia namna ya kutengeneza kingo za bahari ili kuwalina wananchi na changamoto ya maji kuingia kwenye makazi.