Serikali imewahimiza wananchi wafanye usafi na kuacha kutupa taka ovyo ili kulinda mazingira pamoja na kujikinga na magonjwa ya mlipuko yakiwemo kipindupindu.
Wito huo umetolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson mara baada ya kuongoza zoezi la usafi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini lililofanyika katika Kabwe jjjini Mbeya ikiwa ni katika kuelekea kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, leo tarehe 01 Juni, 2024.
Amesema kuwa pamoja na Serikali kuboresha huduma za afya, suala la usafi ni la muhimu hivyo kila mmoja anawajibika kushiriki kikamilifu katika kusafisha maeneo yanayomzunguka.
Mhe. Dkt. Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ameipoongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema hifadhi ya mazingira ambayo inaendelea kuimarika siku hadi siku.
Amesema kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani inaakisi suala zima la upandaji wa miti na hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kupanda miti ili kukabiliana na athari za kimazingira.
Halikadhalika amewataka wananchi walinde mazingira ya milima na waache kufanya shughuli za kibinadamu hususan kilimo au kuchoma moto kwenye maeneo hayo.
iKwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amesema kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani, Ofisi imeratibu shughuli za usafi wa mazingira katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Jiji la Mbeya kutokana na kwamba nchi yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Amesema changamoto za usimamizi na udhibiti wa taka ikiwemo utupaji holela wa taka usiozingatia kanuni, taratibu na miongozo na usimamizi hafifu wa takangumu na maji taka ni mojawapo ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maeneo mengi ya miji na majiji.
Bi. Mndeme amesema takwimu zinaonesha kuwa nchi yetu inazalisha taka takribani tani milioni 7 ambapo kati ya hizo, asilimia 35 pekee hupelekwa dampo.
Amesema hali hii inaweza kuhatarisha afya ya binadamu kutokana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, kuhara, kichocho na magonjwa mengine yatokanayo na ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na kemikali hatarishi.