Serikali imesema inaendelea na majadiliano na wadau mbalimbali zikiwemo kampuni za uzalishaji wa nishati safi ya kupikia ili kupunguza ya gharama za ununuzi wa bidhaa hiyo kwa wananchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo katika tamasha la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia lililoandaliwa na Taasisi ya Upskill Tanzania jijini Dar es Salaam julai 14, 2024.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imekusudia kupunguza gharama za vifaa ili kuhakikisha kila mwananchi bila kujali kipato chake anamudu gharama za nishati safi ya kupikia ambayo ni muhimu na ya lazima kwa kila binadamu.
Mhe. Khamis amesema umaskini mkubwa katika Bara la Afrika, ni wa wanawake kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta nishati isiyo safi ya kupikia itokanayo na kuni nyuma badala ya kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali kiuchumi.
Ameongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya juhudi mbalimbali za kuhamasisha wananchi kutumia nishati ya umeme, gesi na mkaa mbadala ili kuepukana na ukataji wa miti kwa ajili ya kupikia.
“Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan) amekuwa akilifuatilia suala hili la nishati safi ya kupikia tangu akiwa Makamu wa Rais na amekuwa kinara kwa kulisimamia kidete na kulitangaza duniani. Tuendelee kuunga mkono juhudi hizi, kutokana na manufaa yake kwa vizazi vijavyo,” amesema Naibu Waziri Khamis.
Pia, ameitaka Taasisi ya Upskill Tanzania kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa mikoa mbalimbali nchini ili Watanzania wengi waweze kuona umuhimu wa matumizi bora ya nishati safi ya kupikia kwani Tanzania bila nishati ya kuni na mkaa kupikia inawezekana.
Hivyo, amewasihi Watanzania kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi, kuacha kuharibu, kujenga,kulima au kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika vyanzo vya maji.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amesema nishati safi ya kupikia inatambulika kama salama, nafuu, endelevu ambapo dhana yake ni kupunguza athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji.
“Nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu katika kutekeleza maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi na pia ni agenda muhimu katika jumuiya za kimataifa” amesema Mndeme.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2023, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2021.
Ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitekeleza jitihada mbalimbali za kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaimarishwa nchini ikiwemo kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya nishati ya kupikia kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100.
Tamasha hilo lilishirikisha wawakilishi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Benki ya NMB.