Serikali imesema inaendelea na hatua ya kutatua changamoto za Muungano zilizosalia kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameiarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jijini Dodoma leo Oktoba 25, 2024 wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya utendaji wa Ofisi kuanzia Aprili hadi Septemba 2024.
Amesema kuwa lengo la Serikali zote mbili ni kuendelea kuuimarisha Muungano huu adhimu duniani ambao umenufaisha wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Nikuhakikishie Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe changamoto zote zitatatuliwa na ndio maana kupitia busara za viongozi wetu, zikaundwa Kamati kuanzia ngazi ya Wataalamu, Makatibu Wakuu, Mawaziri hadi Kikao cha Kamati ya Pamoja huwa zinakutana kujadili na kutatua changamoto hizi,” amesema.
Pia, Mhe. Naibu Waziri Khamis amesema kupitia Mfuko wa Kuchochea maendeleo ya Jimbo hadi kufikia Juni 2024 shilingi bilioni 2.034 zilipokelewa na kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wa majimbo hayo.
Kuhusu Mazingira, Mhe. Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na utekelezaji wa miradi katika pande zote mbili za Muungano ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametolea mfano miradi ya ujenzi wa matuta na kuta kwa ajili ya kupunguza kasi ya mawimbi ya maji katika pwani ya Bahari kwenye Kisiwa cha Pemba na Mtwara Mikindani.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utendaji kazi wa kuridhisha.
Amesema Kamati hiyo itaendela kutoa ushirikiano kwa vingozi na watendaji wa Ofisi hiyo ili waendelee kutekeleza majukumu yao vyema katika eneo hususan katika usimamizi wa Muungano na Mazingira.
Mhe. Kyombo ambaye pia Mbunge wa Nkenge ameshukuru kwa wajumbe wa kamati yake kukabdihiwa kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo amesema kitatoa elimu tosha kuhusu chimbuko la Ofisi.