Serikali: Tunaendelea kutathmini mabadiliko ya tabianchi

Nov, 07 2023

Serikali imeendelea kuhakikisha inapambana katika utunzaji wa mazingira kwa kupitia sheria, sera na miongozo ya wizara za kisekta ili kutathmini masuala ya mabadiliko ya tabianchi yaliyozingatiwa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Ignas Chuwa wakati akiongoza kikao cha Kamati Tendaji ya Mradi wa Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (NAP) kilichofanyika jijini Dodoma leo Novemba 7, 2023.

Lengo la mradi ni kuimarisha uwezo wa nchi katika kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa kujumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya maendeleo.

Bw. Chuwa amewataka washiriki kutoka wizara za kisekta kutekeleza kazi kuandaa Mwongozo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa kuzingatia muda uliopangwa ili kufanikisha lengo la mradi.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa mradi huo, Bi Asia Akule kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amesema unaandaliwa mifumo ya ufuatiliaji wa mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa fedha.

Pia, Bi. Asia amesema kuwa inafanyika tathmini ya kina kuhusu ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na utoaji wa taarifa zake.

“Kwa sasa tumemaliza hatua ya kwanza ya mradi huu ambao ulianza kutekelezeka Oktoba 2022 na sasa tunaingia hatua ya pili ambapo kiuhalisia hatua ya kwanza ilipaswa kuanza Januari mwaka Jana (2022),” amesema.

Mratibu huyo ameosema kuwa katika mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa sasa hatua ya mwisho katika mpango wa kuomba fedha za awamu ya pili inafanyika.

Mradi wa NAP unatekelezwa kwa kujenga uwezo wa utayari wa nchi katika kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi kupitia mpango wa Taifa wa kuhuisha masuala ya kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi.

Settings