Serikali: Ongezeko la joto duniani ni athari za mabadiliko ya tabianchi

May, 16 2024

Serikali imesema kuwa mojawapo ya athari za mabadiliko ya tabianchi ni kuwepo kwa ongezeko la joto duniani.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema hayo wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo leo tarehe 16 Mei, 2024.

Akijbu swali la Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Mhe. Ameir Abdalla Ameir aliyeuliza ni kwa vipi mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha uvamizi wa wadudu waharibifu kwa mazao mbalimbali, Mhandisi Kundo amesema ongezeko la joto duniani huathiri fiziolojia ya wadudu kwa maana ya mfumo wa ulaji, uzaaji na ukuaji.

Amesema tafiti zimethibitisha kuwa joto na mvua huchochea mabadiliko katika uzaaji, ukuaji na kuenea kwa wadudu waharibifu wa mazao pamoja na magonjwa ya mazao.

“Mheshimiwa Naibu Spika hali hii huchangia ongezeko la aina mbalimbali za wadudu waharibifu wa mazao ambao ni tishio katika uzalishaji na ukuaji wa sekta ya kilimo,“ amesema.

Hata hivyo, Mhandisi Kundo amesema kuna umuhimu wa kuimarisha mifumo na mbinu shirikishi za udhibiti wa wadudu waharibifu ikiwemo ufuatiliaji wa athari za mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa wadudu waharibifu.

Settings