Serikali kuimarisha usimamizi rasilimali za bahari kuongeza wigo wa kunufisha jamii

Nov, 07 2023

Serikali imesema itaendelea kuimarisha sera, mipango na mikakati ya usimamizi wa rasilimali za bahari na kuongeza wigo wa manufaa ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanachama zinazotekeleza Mkataba wa Nairobi.

Rai hiyo imetolewa hivi leo Novemba 7, 2023 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua Warsha ya Kikanda kuhusu Mpango wa Matumizi ya Eneo la Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi iliyoshiriki nchi 10 zinazotekeleza Mkataba wa Nairobi unaohusu Hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi.

Maganga amesema lengo la warsha hiyo ni kujenga uwezo wa wataalamu kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi katika kuandaa na kutekeleza Mpango wa Matumizi ya eneo la Bahari, Usimamizi wa taarifa za kimazingira, kubadilishana uzoefu na kufahamu hatua zilizofikiwa na nchi wanachama katika kuandaa na kutekeleza mpango wa Matumizi ya eneo la Bahari.

Amesema warsha hiyo itasaidia kuandaa mpango na usimamizi endelevu wa matumizi ya rasilimali za bahari ikiwa ni pamoja na mgawanyo sahihi wa matumizi ya bahari na kuongeza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu ambapo imendaa mpango huo kwa kuzingatia kuwa uchumi wa bluu kuwa ni miongoni mwa agenda za dunia.

“Ninapozungumzia uchumi wa bluu ninasisitiza usimamizi endelevu na shirikishi wa mifumo ikolojia ya Pwani na bahari ya Tanzania ili kuendelea kutoa bidhaa na huduma muhimu ikiwa ni pamoja masuala ya uvuvi na uchimbaji wa mafuta na gesi pale vitakakapogundulika,” amesema Bi. Maganga.

Akifafanua zaidi amezitaja nchi zinazotekeleza Mkataba wa Nairobi kuwa ni pamoja na Tanzania, Comoro, Kenya, Somalia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Re-Union na Afrika Kusini ambapo kupitia warsha hiyo wataalamu wa mataifa hayo watajadili ajenda mbalimbali za mazingira na jitihada zinazopaswa kuchukuliwa na nchi wanachama.

Kwa upande wake, Mratibu kutoka sekretarieti ya Mkataba huo, Bw. Dixon Waruinge amesema nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi hazina budi kuwa na mkakati wa pamoja wa usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za bahari katika katika ukanda ya bahari ya Hindi kwa kuwa ni moja ya hatua muhimu ya kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

“Sote ni mashahidi kwa kile kilichotokea kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Madagascar ambazo zilikabiliwa na kimbunga cha Freddy ambacho kilileta madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya binadanu na viumbe hai wengine…Juhudi za pamoja ni muhimu katika kuimarisha hifadhi za bahari” amesema Waruinge

Nae wakilishi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Asili ya Dunia (IUCN) Bi. Minna Epps amesema jitihada za pamoja baina ya wadau wa mazingira bado zinahitaji katika kuhakikisha nchi zote zinaendelea kuweka mkazo katika uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari kuokoa uhai wa rasilimali zilizopo.

Settings