Serikali kuhakikisha mifuko, vifungashio vya plastiki visivyokidhi ubora vinatokomezwa

Jan, 17 2024

Serikali imeendelea kuweka mkakati wa kuhakikisha inazuia matumizi ya mifuko ya plastiki na vifungashio visivyokidhi viwango vya ubora nchini ikiwa ni njia ya kutunza mazingira.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati wa kikao cha 18 cha Wajumbe wa Kikosi kazi cha Taifa cha Katazo la Matumizi ya Mifuko ya Plastiki na Vifungashio visivyokidhi Viwango vya Ubora kilichofanyika Dodoma Januari 17, 2024.

Amesema ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufasaha ni vyema taasisi na wizara mbalimbali kama wadau zishirikiane katika kufanya kazi na kutekeleza yale wanayokubaliana.

“Tuendelea kufanya oparesheni mbalimbali, kusimamia na kukataza matumizi ya vifungashio hivyo pamoja na mifuko ya plastiki sio jambo la mtu mmoja lazima tufanye kazi kama timu,” amesema Bw. Mtawi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Thobias Mwesiga amesema wamekuwa wakipokea taarifa juu ya uwepo wa ongezeko la vibebeo vya plastiki mtaani hali ambayo ni kinyume na kanuni ya usimamizi wa mazingira za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za mwaka 2019.

“Hali hii imesababisha ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na vibebeo hivyo. Kurugenzi ya utekelezaji wa uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira kwa kushirikiana na Kanda ya Mashariki (Temeke, Ilala, Bagamoyo, Mashariki Kusini na Mashariki Kaskazini imeendelea na operesheni maalumu ya katazo kuanzia Januari 5 hadi 15 mwaka huu.

“Zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa mpaka kufikia Januari 17 mwaka huu jumla ya wazalishaji, wasambazaji, na wauzaji 135 walikaguliwa sambamba na masoko,” amesema Dk. Mwesiga.

Ameongeza kuwa jumla ya wasambazaji, wazalishaji na wauzaji 98 wamekutwa na vibebeo/vifungashio visivyokidhi vigezo na kutiwa hatiani huku akiwataka watuhumiwa hao kufika katika ofisi za baraza na kupewa maelekezo pamoja na adhabu kutokana na kosa hilo.

Dk. Mwesiga alifafanua kwamba faini zaidi ya Sh 102 milioni imetozwa kwa watuhumiwa waliohojiwa na kusikilizwa kuanzia Januari mwaka jana huku zaidi ya tani 20 za vifungashio visivyokidhi vigezo vikikamatwa na kuhifadhiwa katika ofisi ya Baraza Mikocheni.

Settings