Serikali: Katazo la matumizi ya kuni, mkaa litazihusu taasisi

Oct, 18 2023

Serikali imesema kuwa katazo la matumizi ya kuni na mkaa litazihusu tu taasisi zote za umma na za binafsi na si kwa mwananchi mmoja mmoja kama inavyotafsiriwa.

Imesema Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024 wakati zile zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku zinapaswa kusitisha matumizi ya nishati hiyo ifikapo Januari 31, 2025.

Akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo lengo la Serikali ni kudhibiti uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti kwa kiwango kikubwa na kulinda afya za wananchi.

“Bahati mbaya sana baadhi ya watu walitafsiri lile tangazo tulilotoa mwezi wa nne wakawa na wasiwasi kuwa sasa itakuwaje hata mama ntilie au majumbani watashindwa kupika, hapana si hivyo lengo letu ni kuanza kwa taasisi zenye watu wengi.

“Ni kweli shule zetu ni watumiaji wakubwa wa kuni, nenda katika taasisi zetu zingine utaona namna gani kuni zinatumika ndio maana tukatoa maagizo haya kwetu sisi wenyewe (taasisi za Serikali na taasisi binafsi) kwanza tuanze kujipanga katika hili na tutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira,“ amesisitiza Dkt. Jafo.

Amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo na matumizi ya muda mrefu wa nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya macho.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019 kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Hali kadhalika inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia kutokana na nishati hiyo kupatikana kwa urahisi na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.

Hivyo, kutokana na athari hizo zilizojitokeza, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda, matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala sanjari na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo.

Waziri Jafo ametoa wito kwa kampuni za gesi, mkaa mbadala na majiko banifu zitumie katazo hili kama fursa ya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa wingi kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko kwa taasisi hizo.

Itakumbukwa kuwa Juni Mosi 2021, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alitoa tamko la Wiki ya Mazingira Duniani na kuzielekeza Taasisi, Mashirika ya Serikali na Sekta Binafsi zianze kutumia nishati mbadala kwa kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji.

Settings