Waziri Jafo ametaja faida za kuwa na maeneo lindwa na nyeti ni kuimarisha uhifadhi wa mifumo ikolojia yenye misitu, vyanzo vya maji na wanyamapori iliyopo nje ya maeneo yanayosimamiwa na sheria nyingine.
Amesema hatua hiyo itasaidia pia Faida nyingine kulinda mazalia, makazi, malisho na makuzio ya viumbe na madhara yatokanayo na majanga ya asili yanayoweza kutokea katika maeneo husika kama vile maporomoko ya ardhi, mafuriko na uvamizi wa wanyamapori.
“Tupo katika hatua ya kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori na wananchi, kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori, uharibifu wa misitu unaotokana na shughuli za kibinadamu kama vile ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni na uchimbaji holela wa madini,” amesisitiza Dkt. Jafo.
Hivyo, amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea na juhudi mbalimbali za kuainisha maeneo mengine, kufanya tathmini na ufuatiliaji na kupendekeza njia bora za uhifadhi katika maeneo mengine yenye sifa za kuwa maeneo lindwa au nyeti
Akiwasilisha taarifa ya Uratibu wa Usimamizi wa Masuala ya Mazingira kwa Wizara za kisekta, mafanikio, changamoto na utatuzi, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuhimiza uanzishaji na kuboresha vitengo vya mazingira katika eneo hilo.
Dkt. Jafo amebainisha kuwa uwepo wa vitengo hivyo umeongeza ushiriki wa wizara hizo katika maandalizi ya mipango, programu na mikakati ya kitaifa inayohusu hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Baadhi ya nyenzo na mikakati mbalimbali ya kitaifa iliyoandaliwa ni pamoja na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Mchango wa Nchi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Taarifa za Hali ya Mazingira Nchini.