Serikali inatambua jitihada za taasisi binafsi katika utoaji wa elimu

Nov, 27 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na taasisi binafsi katika kutoa huduma mbalimbali za jamii ikiwemo elimu.

Amesema hayo wakati akizungumza kwenye Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha mjini Iringa mwishoni mwa wiki ambapo amepongeza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupanua utoaji wa elimu ili kuwawezesha wahitimu kushiriki vyema katika maendeleo ya Tanzania.

Mhe. Khamis amesema elimu ni haki ya kila Mtanzania na wengi hukosa kupata haki hii kutokana na sababu za kiuchumi ndio maana Serikali ililiona hili na ikaamua kutoa elimu bila malipo.

Amesema jitihada za Serikali katika kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ni matunda ya udahili katika chuo hicho na kuwa Serikali itaendelea kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo.

“Nitoe wito kwa uongozi wa chuo kujikita katika kulinda ubora wa elimu inayotolewa pamoja na kuwapatia pia ujuzi na mbinu za kujiajiri ili kuwafanya waondokane na utegemezi wa kuajiriwa kutokana na ukweli kwamba kwa mazingira ya sasa, Serikali haiwezi kuwaajiri wote kwa wakati mmoja,” amesema.

Hali kadhalika Naibu Waziri Khamis ameupongeza uongozi wa chuo kwa hatua ya kuanzisha programu za uuguzi, ukunga pamoja na utabibu akisema itaongeza wataalamu katika hospitali zenye upungufu wa wataalamu.

Hivyo, amewaomba waendelee kuwekeza katika programu zingine za afya ambazo zinaupungufu wa wataalamu huku akisema Serikali itawapa ushirikiano katika kufanikisha adhma hiyo.

Amewataka wahitimu kwenda kuwa imara katika kutumia akili na utashi kujua nini wafanye na kwa wakati gani pasipo kuchagua kazi, ilimradi yenye kipato halali na kwa wanaobaki waendelee kusoma kwa bidii.


Settings