Serikali:Ajenda ya nishati safi ya kupikia inalenga kuokoa mazingira

Jun, 18 2024

Serikali imesema ajenda ya nishati safi ya kupikia inalenga kuokoa mazingira hapa nchini sanjari na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati wa Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema kuwa ni lazima watu wafundishwe namna ya kulinda mazingira na kutumia nishati safi badala ya kuni na mkaa ambayo inatokana na ukataji wa miti kwani bado kuna watu wanaamini ili upike chakula kizuri ni lazima utumie kuni au mkaa.

Mhe. Khamis amesema athari za ukataji miti hazionekani kwa siku moja huku akieleza kuwa mtu anaweza kukata miti miaka 10 lakini athari zake zikaonekana miaka 100 ijayo.

Aidha, Naibu Waziri Khamis amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za kibinadamu zinachangia uharibifu wa mazingira ikiwemo viwanda, mifugo, kilimo, shughuli za uchimbaji madini ambazo pia huathiri vyanzo vya maji.

Amesema bado kuna changamoto ya watu kutiririsha maji machafu kwenye vyanzo vya maji, jambo ambalo linaathiri ikokojia ndani ya vyanzo hivyo hali inayoweza kuathiri afya na mazingira.

Amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ili mazingira ili yawe safi kwani kuna baadhi ya maeneo wapo wanaokiuka sheria na hivyo kusababisha uchafu.

Halikadhalika, amekemea tabia ya baadhi ya watu kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji pamoja na kuwepo kwa sheria inayokataza jambo hilo.

Settings