​Samia: Wanaokata miti kiholela wachukuliwe hatua

Aug, 14 2020

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wananchi wanaofanya vitendo viovu vya ukataji miti kiholela hususan kwenye maeneo ya hifadhi.

Mhe. Samia alitoa agizo hilo katika hotuba yake wakati akizindua Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Alitoa maelekezo kwa wizara yenye dhamana ya misitu na hifadhi isimamie na kuwakuchukulia hatua wale wote wanaoendelea na kilimo kwenye hifadhi za misitu.

“Agizo la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila Wilaya ni agizo halali lililoelekezwa na Ilani yetu ya CCM ya mwaka 2015 katika Ibara 193 (a), hivyo nikumbushe kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri zetu kutekeleza agizo la kupanda miti na kuhakikisha inamea,” alisisitiza.

Aidha, Makamu wa Rais aliitaka jamii kushiriki katika kutunza vyanzo vya maji kwa kutofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji.

Pia alisisitiza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuwa ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu ambapo katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka sh. trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi sh. trilioni 29.5 mwaka 2019.

Aliongeza kuwa sekta hiyo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 mwaka 2018 na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa na hivyo kuchangia upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa wastani wa asilimia 65.

“Aidha, kati ya mwaka 2015 hadi 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 na ukuaji huu wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi unahitaji usimamizi madhubuti katika nyanja za kiutaalam, kisera na kiutendaji,” alisema.

Settings