Rais Samia ayataka mataifa kutimiza ahadi za kutoa fedha za kukabili mabadiliko ya tabianchi

Dec, 01 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyataka mataifa duniani kutambua kuwa suluhisho la uhakika la kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ni kutimiza ahadi za kutoa fedha na kuongeza kasi ya mikakati ya kukabiliana na janga hilo.

Rais Samia ametoa tamko hilo Desemba 01, 2023 katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Amesema ilitolewa ahadi ya dola za Kimarekani bilioni 100 kila mwaka, ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi katika mkutano wa Copenhagen na ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya kiasi hicho kuwa kidogo kuliko kilichohitajika

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema mkutano wa Paris na Ufaransa iliazimiwa kudhibiti ongezeko la joto chini ya nyuzi joto 1.5, lakini hali ni kinyume kwani kasi ya ongezeko la joto kwa sasa duniani inatia wasiwasi.

Rais Samia pia amesema kushindwa kutimiza ahadi kunapunguza mshikamano na imani na kuleta matokeo mabaya kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, ambayo hupoteza kati ya asilimia 2 hadi 3 ya Pato la la Taifa (GDP) kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akisisitiza kwenye mkutano huo, Rais Samia amesema Tanzania ina nia ya kuhamasisha kuongezwa matumizi ya nishati safi na gharama nafuu ya kupikia na teknolojia kote barani Afrika, hasa kwa wanawake.

Settings