Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka wizara za kisekta na taasisi kilichofanyika katika Ukumbi wa Jiji mkoani Dodoma Septemba 2, 2025.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ina dhamana ya kusimamia na kuratibu maeneo mbalimbali ambayo ni Masuala ya Muungano, Hifadhi ya Mazingira, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuai, matumizi endelevu ya rasilimali asilia na uratibu na utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu pamoja na matumizi ya fursa za biashara ya Kaboni.
’’Ukweli usio pingika kuwa Taifa bado linakabiliana na changamoto za kimazingira yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi, kupungua kwa bioanuai, uchafuzi wa mazingira ya mijini na vijijini na matumizi yasiyo endelevu ya bahari, maziwa na mito.
"Ili kutatua changamoto hizi, tunahitaji sera madhubuti, mipango inayotekelezeka na ushirikiano wa pamoja baina ya sekta na taasisi mbalimbali. Aidha, uchumi wa buluu ni eneo jipya na lenye fursa kubwa kwa Tanzania, tukizingatia tunayo bahari ya Hindi, maziwa makuu na mito yenye utajiri wa rasilimali.” Amesema Prof. Msoffe.
Aidha amesema Tanzania imebahatika kuwa na ukanda mrefu wa bahari ya Hindi, maziwa makuu manne, mito na mabwawa makubwa zenye fursa za kipekee zitakazowezesha kukuza uchumi wa buluu kupitia uvuvi wa kisasa, usafirishaji wa majini, utalii wa fukwe, kilimo, ufugaji samaki, na hata nishati jadidifu baharini.
Kuhusu Biashara ya Kaboni amesema lengo ni kuhakikisha kuwa fursa za biashara hiyo inanufaisha watanzania wote na kuvutia uwekezaji katika eneo hilo, ikiwemo misitu, kilimo biashara, usafirishaji, nishati safi ya kupikia, taka ngumu pamoja na maji na usafi (WASH).
Hata hivyo Prof. Msoffe alielezea kuhusu suala la Muungano kuwa ni tunu ambayo waasisi wetu walituachia ambayo tunapaswa kuilinda na kuienzi kwa ustawi na maendeleo ya Nchi yetu.
Amesema matarajio ya Dira 2050 ni kuwa na Muungano imara na thabiti unaoendeleza umoja wa kitaifa, amani, utulivu, na ustawi wa pamoja kwa wananchi wote kuanzia ngazi ya familia.