Ofisi ya Makamu wa Rais yawakaribisha wadau, wananchi Maonesho ya Nanenane 2023 Mbeya

Aug, 02 2023

Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma na Binafsi katika kushiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa jana Agosti Mosi, 2023 na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango yanatarajia kufikia kilele chake tarehe 8, 2023 ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika maadhimisho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya ofisi hiyo ikiwemo elimu masuala ya Muungano na Hifadhi ya Mazingira kupitia Maafisa wa Idara hizo ambao wanatoa ufafanuzi na kujibu maswali mbalimbali ya wateja wanaotembelea banda hilo.

Aidha, katika kuhakikisha elimu ya masuala ya Muungano na Mazingira inawafikia walengwa, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia maonesho hayo imeandaa machapisho mbalimbali ikiwemo vipeperushi, magazeti ya zamani yanayohusu historia ya waasisi wa taifa na masuala mengine ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Elimu ya Muungano itakayotolewa kwa wananchi kwa njia ya maswali na majibu na machapisho mbalimbali ikiwemo ikiwa ni pamoja Kitabu cha “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Chimbuko, Misingi na Maendeleo”, Jarida la Ofisi ya Makamu wa Rais; na Magazeti ya zamani yenye habari kuhusu Muungano.

Kuhusu Mazingira, kupitia maonesho hayo Ofisi inaendelea kutoa elimu kwa wateja na wadau kupitia machapisho mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-2032) unaoanisha hatua na mipango iliyoanishwa na Serikali katika usimamizi bora wa mazingira.

Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na fursa ya Biashara ya Kaboni ni eneo lingine litakalopewa kipaumbele kupitia maonesho ambapo kelimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi na usimamizi wa mazingira itaendelea kutolewa kwa wadau na wananchi kupitia njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari.

Maadhimisho ya Sikukuu ya Nanenane ambayo pia yanaendelea katika mbalimbali nchini yanachagizwa na kaulimbiu isemayo ‘Vijana na Wanawake ni msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.’

Settings