Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha miradi ya mazingira inatekelezwa kwa ubora

Mar, 19 2024

Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itahakikisha miradi ya mazingira inayotekelezwa na Ofisi hiyo inatekelezwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati ili kufikia malengo ya Serikali ya usimamizi endelevu wa mazingira nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Machi 19, 2023 wakati akizindua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia ya Vijijini (EBBAR) Wilayani Mpwapwa, jijini Dodoma.

Mradi huo unasimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) Dkt. Jafo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kulinda mazingira ikiwemo wa EBARR na atahakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo ili iweze kuwa na tija na thamani yake ionekane na kuweza kuwasaidia wananchi.

"Lengo la Rais Samia ni kuona miradi hii inaendelea na kunufaisha watu, hivyo muhakikishe miradi hii inasimamiwa vizuri kwa kuwa inagusa eneo kubwa la maisha ya watu," alisema Waziri Dkt. Jafo.

Naye Diwani wa Kata ya Ngh'ambi, Richard Matonya alisema awali kabla ya mradi huo wananchi walikuwa wanakwenda kuchota maji umbali wa zaidi ya kilometa 10 lakini kwa sasa imesaidia hata kazi za kilimo ambazo wanakijiji hao wamekuwa wakifanya.

Aidha, Mratibu wa EBARR kitaifa, Dkt. Makuru Nyarobi alisema lengo la miradi hii ni kuwasaidia wananchi katika shuguhuli zao hasa katika uchumi ndio maana imejikita zaida katika utekelezaji wake vijijini.

"Kuna wale wakulima walikuwa wanakwenda mbali kutafuta maji lakini sahivi imekuwa tofauti, wakulima nao wamefurahia lakini mafundi cherehani ambao wengi wao ni wakulima wanajipatia kipato kupitia ushonaji," alisema Dkt. Nyarobi.

Mradi wa EBARR unatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya 29,000 na unakadiriwa kuwafikia wanufaika zaidi ya milioni moja (1,000,000) kupitia utekelezaji wa shughuli za miradi mbalimbali kama vile upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kilimo na ufugaji, shughuli mbadala za kujiongezea kipato; na urejeshaji wa vyanzo vya maji. Mradi wa EBARR pia una utekeleza shughuli zake za mradi katika Halmashauri za Kaskazini "A" – Zanzibar na Halmashauri za Wilaya ya Mvomero, Mpwapwa, Simanjiro na Kishapu kwa upande wa Tanzania Bara.

Baadhi ya miradi iliyojengwa kupitia Mradi wa EBARR ni pamoja na Birika za kunyweshea mifugo, Vitalu nyumba, Manzuki (nyumba za nyuki), ununuzin wa Ng'ombe (aina ya Borani), Mbuzi (aina ya Isiolo), Vifaranga vya Kuku, Boti za kisasa za uvuvi zilizonunuliwa Kaskazini A, Visima vya maji pamoja na Shamba Darasa (kwa mazao na ufugaji, uzalishaji wa mbuzi na ng'ombe yameanzishwa, Majosho yaliyojengwa.

Settings