Ofisi ya Makamu wa Rais yapokea Tuzo ya kusimamia mazingira

Nov, 30 2024

Ofisi ya Makamu wa Rais imepokea Tuzo ya kutambua mchango wake katika kuratibu na kusimamia masuala ya mazingira.

Tuzo hiyo imetolewa leo Novemba 30, 2024 wakati wa Mbio za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Change Marathon) wilayani Pangani Mkoa wa Tanga na kupokelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Lengo la mbio hizo ni kuhamasisha jamii kushiriki kwenye shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwa ni hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na mambo mbalimbali, Mhe. Dkt. Kijaji ameongoza zoezi la utoaji wa zawadi kwa washindi wa mbio hizo za marathon na kukabidhi mitungi ya gesi kwa wanawake na watu wenye ulemavu.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Kijaji ameshiriki katika zoezi la kupanda miti aina ya mikoko kwenye kingo za bahari ili kuhifadhi mazingira ya eneo hilo ikiwemo kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi, amesema hiyo ni ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi na kuachana na kuni na mkaa ambazo zina madhara kiafya.

Ametoa wito kwa wanufaika wa mitungi ya gesi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia ili kuwapa hamasa wananchi wengine kuhusu kutumia nishati hiyo na hivyo kusaidia katika kukabiliana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Kijaji amewaonya wazalishaji, waingizaji nchini, wasambazaji na watumiaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali tangu mwaka 2019 akisema inasababisha uchafuzi wa mazingira.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na kutunzwa lakini wapo baadhi ya watu wanarudhisha nyuma juhudi hizo.

Kutokana na changamoto hiyo, amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaouza na wanaotumia mifuko hiyo.

Settings