Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Deogratius Ndejembi amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mkoa wa Dodoma kufanya ukaguzi na kuwakuchukulia hatua watu wote watakaobainika kutililisha maji machafu ndani mifereji ya barabara na kuchafua mazingira katikati ya Jiji.
Akizungumza katika zoezi la usafi wa mazingira leo Juni 03, 2023 jijini Dodoma, Ndejembi amesema wakati wa zoezi hilo imebainika mifereji ya katikati ya jiji hilo imejaa taka ngumu na maji machafu ambayo ni tishio kwa afya ya binadamu.
Ndejembi amesema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitiririsha maji machafu na kutupa taka ngumu katika mifereji ya barabara na kusababisha mifereji hiyo kujaa taka ambazo zinaweza kuleta athari mbalimbali kwa wakazi wa maeneo husika ikiwemo magonjwa ya milipuko.
“Naielekeza NEMC kuja kufanya ukaguzi maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma ikiwemo barabara ya Mwanga baa na barabara nyingine za pembezoni na iwapo mtu atabainika kutililisha maji machafu au taka ngumu kutoka katika nyumba yake au biashara yake hana budi kuwachukulia hatua za kisheria” amesema Ndejembi.
Aidha Ndejembi amewataka wananchi wa Jiji la Dodoma kutenga vyombo maalum vya kuhifadhi taka ngumu ikiwemo chupa za maji pamoja na kutumia magari maalum yanayopita mitaanikwa ajili ya ukusanyaji wa taka ili kuwezesha taka kuteketezwa katika mazingira salama ikiwemo kutupwa katika madampo yaliyotengwa na Halmashauri ya Jiji.
Amesema ni wajibu wa viongozi na watendaji wa mitaa kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha maeneo ya miji kuonekana safi na salama na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Pia, amezitaka Halmashauri za Miji na Majiji kuhakikisha maeneo yote yanayopangwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya wananchi na kuwekewa miundombnu muhimu ya kijamii na kiuchumi kuhakikisha yanapandwa miti ili kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
“Halmashauri hazina budi kuhakikisha kuwa mnapopima viwanja hakuna budi maeneo hayo kupandwa miti ili kuwezesha miji yote kuendelea kuwa ya kijani. Tusipime viwanja na kuwaachia wakazi wenyewe, tuna wajibu wa kuhakikisha barabarani zetu zinapandwa miti” amesema Ndejembi.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Ofisi hiyo itaendelea kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika utunzaji na uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiwemo kuwahamasisha wananchi kujumuika katika kufanya usafi wa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Kilele cha Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yenye kauli mbiu isemayo “Pinga Uchafuzi wa Mazingira unaotokana na Taka za Plastiki” inatarajia kuwa tarehe 5 Juni, 2023 ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
ReplyForward |