Naibu Waziri Kigahe aipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kuandaa kitabu cha Muungano

Aug, 05 2023

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa Kitabu cha Muungano ambacho kitasaidia kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kufahamu chimbuko, historia na mafanikio ya Muungano huo.

Mhe. Kigahe ametoa pongezi hizo leo Jumamosi (Agosti 5, 2023) wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshiriki katika maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Mhe. Kigahe amesema Muungano ni tunu ya taifa ambao umeendelea kudumu kutokana na misingi ya imani, amani, umakini na usikivu wa Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua iliyowezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa baina ya wananchi wa pande zote mbili.

Aidha Naibu Waziri Kigahe ametoa wito kwa wananchi na viongozi kutimiza wajibu wa kuuenzi, kuudumisha, kuuimarisha na kuuendeleza Muungano kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa kutoa elimu kwa vijana inayohusu historia, msingi na chimbuko la Muungano.

Kwa mujibu wa Mhe.Kigahe amesema Kitabu cha Muungano pindi kitakapoanza kufundishwa mashuleni kitakuwa nyenzo muhimu ya msingi wa maarifa na taarifa sahihi kwa wanafunzi kufahamu historia na mafanikio yaliyopatikana katika Muungano.

“Naipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa kitabu hiki ambacho kimekuja kwa wakati mwafaka kwani kitawezesha vijana wetu kuweza kujifunza na kuelewa kwa mapana historia ya Muungano wetu ambao umeleta mafanikio lukuki kwa wananchi wa pande zote mbili” amesema Mhe. Kigahe.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu, Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais alimshukuru Naibu Waziri Kihage kutembelea Banda la Ofisi hiyo kwani kupitia maonesho hayo elimu ya masuala ya Muungano na Mazingira imeendelea kutolewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kukuza uelewa wa pamoja.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kigahe amepongeza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuhamasisha juhudi za utunzaji na uhifadhi wa mazingira kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi kushiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”

Settings