Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa Serikali za Mitaa kote nchini kusimamia kikamilifu Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ili kuzuia shughuli za kibinadamu.
Amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 07 Juni, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Mhe. Askofu Josephat Gwajima aliyetaka kujua mpango gani wa dharura wa kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika jimbo hilo.
Mhe. Khamis amesema shughuli za kibinadamu hasa uchimbaji wa mchanga zinachangia uharibifu wa mazingira.
Kutokana na hali hiyo amezitaka halmashauri kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira ili kudhibiti upanukaji wa mito na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis amesema katika kukabiliana na changamoto za kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi wa Jimbo la Kawe, Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Bonde la Wami-Ruvu Aprili, 2024 iliingia mkataba na Kampuni ya Meg Business Solution Limited kwa ajili ya kusafisha mchanga, tope, taka ngumu na kudhibiti mmomonyoko wa kingo za Mto Mbezi eneo la Ukwamani Mzimuni.
Ameongeza kuwa katika mkataba huo, ufukwe uliopo Mtaa wa Mbezi A Kata ya Kawe utasafishwa mchanga ambapo hadi sasa shughuli hizo zinaendelea.