Naibu Waziri Khamis awatembelea waathirika wa mafuriko Katesh

Dec, 12 2023

Serikali imesema itafanya utafiti katika sehemu ya ardhi iliyoathirika na mafuriko Katesh wilayani Hanang Mkoa wa Manyara kama itafaa kwa matumizi ya kilimo na ufugaji.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alipofanya ziara ya kukagua athari zilizotokea wakati wa maafa hayo yaliyotokea Desemba 03, 2023.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni mratibu wa shughuli zote za mazingira itatumia watalaamu wake kuona namna gani inaweza kuirejesha ardhi hiyo ili iweze kuzalisha.

Pia, Naibu Waziri Khamis amewapa pole walioathiriwa na mafaa hayo akisema kuwa Serikali iko makini na inaendelea kushirikiana na wananchi wa Hanang katika kipindi hiki na kuwawezesha kurejesha katika hali ya kawaida.

Mhe. Khamis amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliamua kuahirisha safari yake Dubai alipokuwa akishiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi na kurejea nchini kuwatembelea na kuwafariji waathirika kwa maafa hayo.

Naibu Waziri amewapa pole waathirika hao wakiwemo waliopoteza ndugu na mali zao na kuwaomba wawe na moyo wa subira na kumshukuru Mungu katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.

“Nimekuja kuwapa pole kwa maafa haya yaliyotokea, Serikali ipo nanyi na inaendelea kuwapatia huduma zikiwemo makazi ili mrejee katika hali mliyokuwa nayo mwanzoni,“ amesema.

Aidha, Naibu Waziri amewaomba wananchi kumshukuru na kuendelea kumuomba Mungu na kuwa na moyo wa subira ambapo amewatia moyo kwa yote yaliyotokea.

Ametoa wito kwa uongozi wa wilaya kuendelea kuwapa ushirikiano waathirika ambao idadi kubwa ni wanawake, wazee na watoto ikiwemo kufuatila familia zilizoathirika popote zinapokuwa ili ziendelee kupatiwa misaada.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Janeth Mayanja na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya.

Mara baada ya kutokea kwa maafa hayo Serikali ilichukua hatua za haraka zikiwemo kuwapa hifadhi waathirika katika Shule ya Sekondari Katesh na kuendelea kuwapatia huduma.

Settings