Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa wananchi kutofanya shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ya bahari na badala yake waitunze.
Ametoa wito huo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino ya Kata ya Mohoro katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Agosti 16, 2024.
Mhe. Khamis pamoja na kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko, amewaomba wananchi wananchi kuacha kuvua kwa kwa kutumia uvuvi usio rasmi ambao unachangia kuua viumbe vya baharini na makazi ya samaki.
Amewataka wananchi kuacha kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuchoma misitu na kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa kwani vitendo hivyo vinaharibu mazingira na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huleta mafuriko.
“Ndugu zangu twendeni tukapande miti kwa wingi na kuitunza, haiwezekani tuhimize upandaji wa miti halafu tena tuikate, nawaomba tuache kuchoma misitu tunaharibu mazingira, uchumi na afya zetu, matarajio ni kuanza kutumia nishati safi ya kupikia na sio tena kuni na mkaa kwani matumizi hayo yana madhara kimazingira na kiafya pia, amesisitiza Mhe. Khamis.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Jackson Kiswaga kwa upande wake amesema mabadiliko ya tabianchi ni janga la kidunia na taarifa hizi za tahadhari zinazotolewa wananchi wazifuatilie.
Amesema kwa mujibu wa tafiti joto linaongezeka hali inayowezeka kusababisha mvua zilizozidi kiwango na hivyo kuleta nafuriko katika siku za usoni hivyo ametoa wito wa kuendelea kuwafikisha wananchi elimu ya mazingira.
“Tumepokea taarifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais inaonekana eneo hili ni la mkondo wa maji na ndio maana Serikali imechukua hatua ya kutenga eneo linguine kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na mafuriko,” amesema.
Aidha, Mhe. Kiswaga amewaomba wananchi waliokwisha kupatiwa maeneo mengine na Serikali waanze kujenga makazi na kuhama katika eneo hilo na kuhamia katika maeneo salama zaidi.
Halikadhalika, mwnyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Kalenga ametoa wito kwa wananchi kutumia majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo ha tua itakayopunguza vitendo vya ukataji kuni taratibu hadi kufikia mwaka 2020 matumizi hayo yawe mwisho kabisa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge ameishukuru Serikali kwa kutoa tahadhari mapema kuhusu kutokea kwa changamoto hiyo na hivyo madhara kutokuwa makubwa.
Amesema wilaya za Mkoa wa Pwani zilizoathiriwa na kimbunga Hidaya uongozi wa mkoa ulichukua tahadhari mapema kwa kukagua na kuwatahadharisha wananchi ili kuepukana madhara makubwa.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msaada wa vyakula pamoja na viongozi wengine akisema hatua hiyo imeleta faraja kwao.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Kasalali Mageni na Mhandisi Stella Manyanya wameshauri wananchi waliopatiwa maeneo waanze kuhamia na kuliacha eneo lililoathiriwa kwa mafuriko.
Wajumbe hao wamesema kuwa pia maeneo mapya wanayohamishiwa wananchi hao yasiwe tena yenye kuchangia uharibifu wa mazingira na kusababisha athari zingine.
Katika ziara hiyo wajumbe hao wametembelea na kukagua maeneo yaliyoathirikiwa na athari hizo yakiwemo Shule ya Msingi Mohoro, daraja na kituo cha afya
Itakumbukwa kuwa kati ya Machi na Aprili 2024 Wilaya ya Rufiji ilikumbwa na mvua za El nino zilizosababisha jumla ya kaya 23,360 kukosa makazi ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na taasisi zingine ilichukua hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo.