Naibu Waziri Khamis ataja Mafanikio baada ya utatuzi wa changamoto za Muungano

Nov, 08 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema mafanikio ya utatuzi wa changamoto za Muungano ni ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa katika maeneo ajira kwa Watumishi wa Zanzibar wanaofanya kazi katika Taasisi za Muungano, wameendelea kunufaika na ajira hizo ikiwa ni asilimia 79 kwa Tanzania bara na 21 kwa Zanzibar.

Amesema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mohamed Said Issa aliyetaka kujua mafanikio baada ya utatuzi wa changamoto za Muungano, bungeni jijini Dodoma leo Novemba 8, 2023.

Pia, Mgawanyo wa Fedha za Mapato yatokanayo na Misaada na Mikopo Nafuu ya Kibajeti (GBS) imeendelea kuongezeka tangu kupatiwa ufumbuzi wa kero hii na kuendelea kuimarisha Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano.

Naibu Waziri Khamis amesema tangu kuasisiwa kwa Muungano Serikali zliona haja ya kuunda kamati ya kutatua changamoto katika ngazi mbalimbali.

Amesema kuwa kamati hiyo inafanya vizuri ndio maana yamepatikana mafanikio makubwa katika utatuzi wa changamoto za Muungano akiyataja mengine kuwa ni Kodi ya Mapato yatokanayo na mishahara ya watumishi wa Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.75 kimekuwa kikitolewa kwenda SMZ kila Mwezi kuanzia Mwaka 2012/13 kama malipo ya PAYE.

Hali kadhalika mafanikio mengine ni Kampuni zilizosajiliwa Tanzania Bara na zenye matawi Zanzibar zimeanza kulipa Kodi ya Zuio (Withholding Tax) kwa upande wa Zanzibar. Vilevile, mapato yanayotokana na Tozo za VISA kutumika pale yalipokusanywa kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano.

“Kulikuwa na hoja kwamba wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, suala hili limepatiwa ufumbuzi na sasa wafanyabiashara hulipa kodi inayostahili kwa tathmini ya bidhaa inayotumika Tanzania Bara. Kwa muktadha huo, suala la ulipaji wa tofauti ya kodi kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara linaeleweka vizuri kwa wafanyabiashara wa Zanzibar,“ amesema Naibu Waziri Khamis.

Settings