Naibu Waziri Khamis aiasa Jamii kuchukua tahadhari dhidi ya Ukimwi

Oct, 12 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu alipotembelea na kujionea shughuli zinazoratibiwa na ofisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana na Wiki ya Kimataifa ya kupunguza madhara ya maafa yanayoendelea katika viwanja vya Stendi ya zamani ya mabasi Babati.

Naibu Waziri Khamis amesema jamii haina budi kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini ipungue na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.

“TACAIDS imeendelea kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu, ila endeleeni kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea maendeleo yetu, hivyo elimisheni kwa nguvu watu wabadili mitazamo yao,” alisema Mhe. Khamis.

Aliongezea kuwa, Tume iendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Kondomu ili kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI hasa kwa kundi la vijana nchini.

“Endeleeni kufunga makasha ya kondomu katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo; kumbi za burudani, baa na nyumba za wageni lengo ni kuendelea kupunguza maambuki ya VVU na UKIMWI,” alisisitiza.

Kwa upande wake Mratibu wa UKIMWI kutoka TACAIDS Bw. Gilbert Mbwambo akieleza majukumu ya Tume hiyo alisema kuwa Serikali imeboresha huduma za VVU na UKIMWI ikiwa ni pamoja na utoaji wa dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI kwa watu wenye maambukizi ya virusi hivyo pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya Kondomu.

Settings