Naibu Waziri Khamis ahimiza kila mwananchi ashiriki zoezi la usafi

Sep, 21 2024

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema suala la usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja ambalo anapaswa kulitekeleza.

Ametoa kauli hiyo wakati akiongoza wananchi kufanya usafi katika eneo la Soko la Mavunde, Chang’ombe jijini Dodoma kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani leo Septemba 20, 2024.

Mhe. Khamis amewahimiza wananchi kufanya usafi katika makazi yao na maeneo ya biashara, zoezi ambalo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya binadamu ili kukabiliana na maradhi.

Ameongeza kuwa si vizuri kuacha taka zikazagaa ovyo huzalisha bacteria na pia kusababisa changamoto mbalimbali zikiwemo kemikali hatarishi kwa binadamu na viumbe hai wengine.

Amewaomba wananchi kuunga mkono maelekezo ya Serikali kufanya usafi wa mazingira hususan kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na siku zingine ili kuweka miji katika hali ya usafi.

“Mnakumbuka Rais wetu kila anaposimama kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali, anazungumzia usafi wa mazingira hivyo nasi hatuna budi kumuunga mkono katika jitihada hizo,” amesisitiza Naibu Waziri Khamis.

Halikadhalika, amesema watalii wanaokuja nchini kuangalia vivutio wanahitaji kukuta hali ya usafi hivyo kuvutiwa na kuitangaza zaidi nchi hatua itakayohamasisha watalii kuja kwa wingi.

Kwa upande wake Mratibu wa Kampeni ya Mtu ni Afya kutoka Wizara ya Afya Bw. Anyitike Mwakitalima Siku ya Usafi Duniani inahusiana moja kwa moja na na suala la afya ambayo ina dhamana ya kudhibiti magonjwa.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Uhai hauna mbadala zingatia usafi wa mazingira’ inadhihirisha kuwa ili tuwe hai tusipate maradhi lazima watu wazingatie usafi wa mazingira.

Aidha, Bw. Mwakitalima amepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali kwa ujumla na wananchi wa eneo la Chang’ombe kwa kushiriki katika zoezi la usafi kuzunguka soko hili hatua itakayoamsha ari kwa wananchi wengine kufanya usafi. Ametoa wito kuwa zoezi la usafi lisiishie kufanyika tu Siku ya Usafi Duniani bali liwe endelevu.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya GoPlant Bw. Emmanuel Likuda iliyoandaa zoezi hilo amesema Siku ya Usafi Duniani inatambuliwa na Umoja wa Mataifa na inafanyika katika nchi nyingine duniani.

Settings