Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa wakulima na wafugaji nchini kufanya shughuli zao bila kuharibu mazingira.
Ametoa wito huo leo Novemba 28, 2024 jijini Dodoma wakati akiongoza kikao na Ujumbe wa Tanzania ambao utashiriki katika Mkutano wa 16 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame ambao unatarjiwa kufanyika katika Jiji la Riyadh nchini Saudi Arabia.
Mhe. Khamis amesema vitendo vya baadhi ya wakulima kukata miti ovyo na kuchoma misitu kwa ajili ya kuandaa na kusafisha mashamba na wafugaji kulisha mifugo kiholela huchangia ukame na hatimaye kuwepo na tishio ya maeneo mengi kuwa jangwa.
Aidha, Naibu Waziri amewasihi wakulima na wafugaji kuacha kuhamahama kwani kitendo hicho kinachochea hatari ya kuenea kwa jangwa.
"Wakulima na wafugaji wanapokata miti na kulisha mifugo wanapohamahama wanaacha maeneo yakiwa yameharibiwa, hivyo nawaomba waache kufanya hivyo wanasababisha maeneo mengi kukabiliwa na hali ya ukame na jangwa," amesisitiza.
Mhe.Khamis amesema pamoja na kuwa ufugaji na kilimo ni sekta kubwa zinazokuza uchumi na kutangaza nchi yetu wafugaji na wakulima wanao wajibu wa kuhakikisha wanafuata sheria za mazingira na hivyo kupunguza ongezeko la jangwa.
Halikadhalika, amewaomba wafugaji waache kuchunga au kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji kwani kwa kufanya hivyo wanasababisha uharibifu wa mazingira maji kukauka na kuleta ukame.
Aidha, naibu waziri huyo amewasisitiza wafugaji na wananchi kwa ujumla kupanda miti na kuitunza ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba nchi yetu.
Amesema hali ni mbaya kwasababu maeneo mengi wananchi wamekata miti ovyo hali inayosababisha ukosefu wa mvua na hivyo ukame kukithiri katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Hivyo, Mhe. Khamis amesema ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira amesema Serikali itaendelea na jitihada za kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema mkutano huo wa kupambana kwa hali ya jangwa ni muhimu kwa Tanzania.
Amesema kama Tanzania kupitia wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo itakuwa katika nafasi nzuri ya kushiriki kikamilifu kwa mustakabali wa nchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Bi. Agnes Meena na wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wizara za kisekta na Mkurugenzi wa Taasisi ya LEAD Foundation Bw. Njamasi Chiwanga.