Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa wito kwa wadau wa kampuni mbalimbali kuendelea kulinda na kuhifadhi mazingira.
Bi. Mndeme amesema hayo jijini Dodoma Juni 27 ,2024 alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Belta Waste Paper Recyclers Bi. Belta Kazimoto na kumpongeza kwa juhudi ya wanayofanya katika utunzaji na uhifadhi wa Mazingira, Dodoma.
Belta Waste Paper Recyclers inajihusisha na utunzaji wa mazingira kwa uchakataji wa takataka unaotokana na karatasi kwa kuziongezea thamani na kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vitabu na kalamu ambazo zimewekwa mbegu za matunda ambapo mwisho wa matumizi huoteshwa.
Bi. Mndeme ameongeza kuwa kampuni hiyo inafanya kazi kubwa ya kuungana mkono juhudi za Mwanamazingira namba moja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutunza mazingira.
“Pamoja na utunzaji wa mazingira lakini kampuni hiyo imeajiri wanawake hivyo ni jambo la kuwapongeza watu wanaofanya jitihada za namna hii kwa kuhakikisha wanalinda mazingira yetu.
“Kitendo wanachokifanya wanapunguza utoaji wa hewa joto kwenye anga, tunaposoma magazeti au kampuni za magazeti zinapomaliza kuuza kuuza bidhaa zao na yale mabaki badala ya kuchoma kampuni hii inabadilisha zile karatasi na kuwa pesa kwa kutengeneza bidhaa hizi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Belta Waste Paper Recyclers Bi. Belta Kazimoto amesema chanzo kikubwa cha ukusanyanyi wa karatasi wanazotumia ni kutoka shuleni na ofisini.
“Tumekuwa tukitembea ofisini na kuzikusanya taka za karatasi hivyo badala ya kuzichoma tunazikusanya na kuzichakata na kuwa bidhaa ikiwa moja ya jitihada za kutunza mazingira yetu,” amesema Bi. Kazimoto.