Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme inakadiriwa kuwa asilimia 61 ya ardhi iko katika hatari ya kuharibika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema maeneo ya nchi yenye hali ya mvua chache yamezidi kukumbwa na ukame na hivyo kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na kutishia usalama wa chakula katika maeneo hayo.
Bi. Mndeme amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) leo Juni 24, 2024 kinachofanyika jijini Mbeya kwa siku tatu huku akionesha kuridhishwa na utekelezaji wake na kuwapongeza wataalam wanaoutekeleza.
Amebainisha kuwa uharibifu huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na uwezo wa malisho, ukataji misitu, ukataji wa misitu kwa ajili ya kuni na mkaa, ufunguaji mashamba mapya unaotokana na kilimo cha kuhamahama, mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji holela wa madini.
Bi. Mndeme amesisitiza kuwa mradi huo unaendeleza juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira kwa kurejesha ardhi iliyoharibika na kujengewa uhimilivu wa mfumo wa ikolojia na jamii kwa ujumla.
“Nimejulishwa kuwa mradi huu umezingatia maslahi, mahitaji halisi na vipaumbele vya taifa letu sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Pia nimejulishwa tupo nyuma ya ratiba ya utekelezaji wa shughuli za mradi kutokana na kuchelewa kuanza kwa shughuli za mradi, hata hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitoa fedha kwa wakati ili tuweze kuendana na ratiba,” amesema Bi. Mndeme.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo Dkt. Damas Mapunda amesema umesaidia hasa jamii zile zinazojihusisha na kilimo, pamoja na ufugaji katika kujifunza namna ya kulinda nma kutunza mazingira.
“Tumekuwa tukijitahidi kutoa elimu kila wakati ili kuona namna elimu inakwenda kwa wengi ili kuhakikisha lengo letu la uhifadhi na utunzaji wa mazingira linafanikiwa kwa asilimia kubwa,” amesema Dkt. Mapunda.