Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amezipongeza taasisi ambazo zinatumia nishati safi ya Kupikia kwa vitendo zikiwemo majeshi na wizara.
Ametoa pongezi hizo alipokuwa kwenye ziara ya uelimishaji umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji mazingira katika Chuo cha Mafunzo Zone ya Kiinua Miguu Kilimani, Zanzibar Agosti 24, 2024.
Ameongeza kuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limekuwa mfano wa kuigwa baada ya kambi zake nyingi kwa sasa hutumia mfumo wa nishati safi ya kupikia na kuanchana na matumizi ya kuni na mkaa ambao ni hatari kwa mazingira.
“Nizipongeze taasisi zote kikiwemo Chuo cha Mafunzo Zanzibar kwa uamuzi waliouchukua wa kutumia nishati safi, ni ukweli kwamba wameona faida nyingi katika matumizi ya nishati safi tofauti na awali.
“Wizara ya Elimu kuna baadhi ya shule na vyuo wanatumia Nishati safi vivyo hivyo, Wizara ya Afya kuna hospitalini sasa wanatumia nishati safi japo sio zote hivyo naamini hadi Agosti 30, 2024 wengi watakuwa wamehama kama ilivyoelekezwa na viongozi wetu,” amesema Bi. Mndeme.
Ameongeza kuwa vyuo vya Mafunzo vinapaswa kuiga mfano wa Chuo cha Mafunzo Kilimani sababu hakuna haja ya kuendelea kutumia kuni na mkaa katika nyakati kama hizi.
Kwa upande wake, Mkuu wa chou hicho SSP- Mrakibu Mwandamizi Amour Naimu Khamis amesema wameiona faida kubwa katika matumizi ya Nishati safi ya kupikia sababu gharama walizokuwa wakitumia zamani na sasa kuna utofauti mkubwa.
Amesema kabla ya kuanza kutumia mfumo huu, walikuwa wanatumia kuni tani 50 kwa mwezi lakini kwa sasa wameacha baada ya kupata mfumo mpya wa matumizi ya nishati safi