Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wanatenganisha mfumo wa maji machafu na mfumo wa maji masafi (mvua) yanayoingia katika Bahari ya Hindi.
Bi. Mndeme amesema hilo ni jukumu la DAWASA katika kuhakikisha mifumo hiyo inajitegemea maana eneo hilo limekuwa na lawama nyingi kutoka kwa wananchi kutokana na harufu mbaya inayotoka katika fukwe eneo la Aga Khan hadi Ocean Road.
Amesema hayo wakati ziara yake ya kikazi katika fukwe ya Bahari ya Hindi eneo la Aga Khan hadi Ocean Road jijini Dar es Salaam, Machi 26, 2025 ambapo amesisitiza kila mmoja anapaswa kuwajibika kwani eneo hilo kwani suala la mazingira linamgusa kila mtu.
Bi. Mndeme pia ameielekeza DAWASA kuyatibu maji machafu katika vituo vyao kabla ya kuingia katika mifumo ya maji machafu ili yanapoingia baharini yawe yametibiwa sababu bahari inategemewa katika shughuli nyingi za uchumi na jamii.
“Tunahitaji tulinde mazingira ya bahari hivyo nawaelekeza tena DAWASA kujenga eneo la kutibu maji machafu ili yale yanayokwenda baharini yawe yametibiwa kwani hilo litasaidia kulinda viumbe hai waliokuwa baharini, kuondoa au kupunguza harufu pamoja na kupunguza magonjwa.
“Tumegundua maji yanayokwenda baharini kupitia mfumo wa DAWASA hayana tiba, hivyo ule uchafu unakwenda kama ulivyo, hivyo wanapaswa kujenga haraka kituo cha kutibiwa maji machafu,” amesema Bi. Mndeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ilala Mhe. Elihuruma Mabelya wajibu wa jiji ni kulinda mazingira ili yawe safi na salama na kama alivyoongea Naibu Katibu Mkuu (Mndeme) hapa kuna tatizo ambalo linagusa pande mbili.
“Upande wa kwanza unagusa wananchi ambao wanaunganisha maji taka kwenye mfumo wa maji safi ambapo kimsingi ni ndio unasababisha tatizo hili la harufu mbaya na uchafuzu wa mazingira na bahari na upande wa pili ni sisi kama halmashauri ya Dar es Salaam ambao tunasimamia mfumo wa maji ya mvua, hivyo ni wajibu wetu sisi na DAWASA kuona namna gani tunaondoa tatizo hili,” amesema Mabelya.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi. Everlasting Lyaro akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA amesema ni kweli kuna changamoto ya kimfumo baada ya kugundua watu wamejiunganishia maji machafu kwenye mfumo wa maji ya mvua na tayari mikakati imewekwa kwa ajili ya kudhibiti tatizo hilo.