Naibu Katibu Mkuu Mndeme aahidi kusimamia matumizi ya nishati safi ya kupikia

Mar, 13 2024

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ameahidi kushirikiana na viongozi pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo kusimamia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanahama kutoka katika nishati isiyo safi ya kupikia kwenda katika nishati safi na salama ifikapo mwaka 2030.

Bi. Mndeme amesema hayo wakati alipojitambulisha kwa Viongozi wa Ofisi ya Makamu wakiongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis na Katibu Mkuu, Bi. Mary Maganga muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo leo Machi 13, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda muhimu ya kimkakati inayolenga kumkomboa mwanamke wa Kitanzania na kutokana ambapo kutokana na umuhimu huo Serikali imeweka mazingira wezeshi na rahisi ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ikiwemo kupunguza gharama za ununuzi wa gesi.

“Mwishoni mwa wiki iliyopita wakati tukisherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani, tumeshuhudia kongamano kubwa la masuala ya nishati safi ya kupikia na maelekezo na mahsusi ya viongozi yametolewa, hili ni agizo ambalo halina budi kusimamiwa” amesema Bi. Mndeme.

Aidha ameeleza kuwa atatumia uzoefu alionao katika kusimamia majukumu ya ofisi yake ambapo ameahidi ushirikiano baina yake na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais ili wadau na wananchi wa makundi mbalimbali kuweza kupata huduma bora inayotolewa na ofisi hiyo.

Ameongeza kwa kuzingatia msingi wa majukumu ya ofisi hiyo amejiwekea utaratibu wa kupokea ushauri na mapendekezo ili kuimarisha mfumo wa utendaji kazi na kuleta tija iliyokusudiwa na jamii kwa kuwa na Tanzania yenye Muungano imara, Mazingira safi, salama na endelevu kwa ustawi wa jamii.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amempongeza Bi. Mndeme kwa uteuzi huo kwani imeongeza nguvu katika safu ya uongozi ndani ya ofisi hiyo imekamilika katika utekelezaji wa majukumu yake kwa umma wa Watanzania.

“Natumai kwa kipindi ulichohudumu ndani ya Serikali utakuwa ni chachu ya mageuzi ya kimkakati utendaji kazi wa ofisi yetu ambayo ina dhamana kubwa ya kudumisha Muungano wetu na sambamba kulinda mazingira” amesema Mhe. Naibu Waziri Khamis.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga ameahidi kutoa ushirikiano kwa Naibu Katibu Mkuu Mndeme katika kutekeleza majukumu ya kiofisi kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza tija ya Ofisi hiyo katika kuwahudumia wananchi.

Settings