Mradi wa urejeshwaji wa mazingira kupanuliwa

Mar, 15 2025

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema ofisi hiyo imekusudia kuongeza wigo wa maeneo ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR-Tanzania) ikihusisha Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji.

Mhandisi Luhemeja amesema hayo leo Machi 15, 2025 Jijini Mbeya wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati tendaji ya kitaifa ya usimamizi wa mradi huo kilichojadili shughuli za utekelezaji wa mradi hadi kufikia sasa.

Luhemeja amesema tathimini iliyofanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mikoa na Halmashauri zinazotekeleza mradi huo, imeonesha wananchi wengi wamefurahishwa na utekelezaji wa shughuli za mradi na hivyo Serikali imepanga kuhakikisha kuwa inaongeza wigo wa maeneo ya utekelezaji wake.

“Mwezi Oktoba mwaka huu tutafanya tathimini ya mradi na ili kuona uwezekano kupata maeneo mengi zaidi ya utekelezaji na kuwanufaisha wananchi kwani wengi wao wamevutiwa na fursa zitokanazo na uhifadhi endelevu wa mazingira kupitia shughuli mbadala za kiuchumi” amesema Luhemeja.

Ameongeza kuwa kupitia mradi wa SLR Serikali, imepanga kubuni miradi mingi zaidi ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya kusaidia jamii na hivyo kuongeza hamasa kwa jamii kutumia vyema fursa ya mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kuibua fursa mbalimbali.

Amefafanua kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kujenga uwezo kwa jamii zinazotekeleza mradi huo ziweze kuhamasisha katika masuala ya uhifadhi wa mazingira na kutumia fursa zilizopo kuweza kujiongeza kipato kupitia shughuli za uzalishaji mali.

“Tumeona Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mpimbwe wananchi wamehamasika kupanda miti na kuingia katika biashara ya kaboni na hivyo kujiongeza kipato.....Tumejipanga kuhakikisha fursa hizi pia zinaweza kuwanufaisha wananchi wa maeneo mbalimbali nchini” amesema Mhandisi Luhemeja.

Ameeleza kuwa kupitia mradi wa SLR wananchi wameweza kutumia mbinu za kisasa za uzalishaji mali ikiwemo kilimo rafiki kwa mazingira ambacho kimewazesha wananchi kuweza kuvuna kiasi kikubwa cha mazao na kujiwekea akiba kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo mbegu bora na teknolojia ya umwagiliaji.

Aidha Luhemeja amezihimza jamii zilizonufaika na mradi huo kutumia vyema rasilimali zilizopo ili kuwa endelevu sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kutunza na kuhifadhi mazingira kwani Serikali itaendelea kutafuta fedha fedha za kuwezesha miradi mbalimbali ya mazingira.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR), Dkt. Damas Mapunda amesema mradi huo umekuwa mkombozi kwa jamii zilizoathirika na uhalibifu wa mazingira kwa kuwapatia shughuli mbadala kwa ajili ya uzalishaji mali.

“Mradi huo umepata ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wake kutoka katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, hatua inayowezesha Serikali kuweza kufikia malengo iliyojiwekea ya urejeshwaji wa uoto wa asili katika maeneo mbalimbali nchini” amesema Dkt. Mapunda .

Ameongeza kuwa hadi kufikia sasa mradi huo umefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kukamilisha mradi huo kwa kwa wakati na viwango vilivyokusudiwa.

Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji. Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na unatarajia kukamilika mwaka 2025 na ambapo jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54 zinatarajia kunufaika.

Halmashauri hizo ni Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga Vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.

Settings