Mkakati wa muda mrefu wa upunguzaji wa gesi joto waiva

Aug, 14 2024

Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau ikiwemo wizara za kisekta iko katika hatua za awali za kuandaa Mkakati wa muda mrefu wa upunguzaji wa gesi joto.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko Ya Tabianchi (Cop-28), Uliofanyika Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 Dubai, Falme Za Kiarabu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Agosti 14, 2024.

Amesema nchi wanachama zimekubaliana kupunguza ongezeko la gesi joto duniani kwa lengo la kuhimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutekeleza mwongozo unaobainisha mwelekeo wa kuwezesha jitihada za kuhimilili changamoto hiyo nchini.

Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa Mapitio ya Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi yameanza ambapo kwa sasa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) inafanya tathmini ya uzalishaji wa gesi Joto. Sekta zinazohusika ni pamoja na Nishati, Usafirishaji, Udhibiti wa taka, na Misitu.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kuwa ugawaji wa mitungi na majiko ya gesi uandane na elimu ya mazingira.

Amesema ni muhimu kutoa kuwaelimisha wananchi athari za matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na badala yake nishati safi ichukue nafasi katika shughuli za upishi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja kwa upande wake amesema suluhisho la ukataji wa miti ni biashara ya kaboni kupanda miti kutumia nishati safi ni suluhisho la ukataji miti

Pia, amesisitiza umuhimu wa kusukuma ajenda ya upandaji wa miti na kuitunza kwa jamii ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan ukame.

Amesema pamoja na hayo pia ni muhimu ya kuwaelimisha umuhimu wa matumizi ya majiko banifu ambayo yatasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kupitia kwa Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga imetaka kuona wananchi wananufaika na fedha zinazotokana na mfuko wa mazingira hasa kupitia miradi ya maendeleo.

Halikadhalika wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Dkt. Bashiru Ali, Mhe. Agnes Hokororo wamesisitiza kuwa umuhimu wa ushirikano na wizara na taasisi katika tafiti za mazingira.

Pia wamesisitiza kuwa ugawaji wa vifaa vya nishati safi ya kupikia ufanyike zaidi katika maeneo ya vijijini ambako changamoto ya uharibifu wa mazingira ni kubwa.

Settings