Mitawi: Kazi kubwa inafanyika katazo la mifuko ya plastiki

Sep, 29 2023

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha juhudi za kuzuia matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango vya ubora zinafanikiwa.

Ameeleza hayo Dodoma Septemba 29, 2023 katika kikao cha 17 cha Kikosi kazi cha Taifa kinachoratibu na kusimamia Utekelezaji wa Marufuku ya Mifuko ya Plastiki Tanzania Bara kuhusu tathmini ya matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango vya ubora.

Bw. Mitawi amesema licha ya mafanikio hayo lakini kuna changamoto katika utekelezaji wa marufuku hiyo kwasababu watu binafsi, kampuni na taasisi zinashindwa kutekeleza kwa ufanisi marufuku hiyo.

“Elimu inatakiwa zaidi juu ya marufuku ya matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango vya ubora kwa wananchi na mamlaka zinazohusika na utunzaji wa mazingira ili tuweze kufanikiwa,” amesema Mitawi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi Kemilembe Mutasa amesema maafisa mazingira wanapaswa kuweka mikakati ya namna ya kusimamia tamko la Waziri la marufuku ya vifungashio vya plastiki katika maeneo yao.

Pia, amesema zoezi la ukaguzi katika masoko na sehemu za kuuzia vyakula linapaswa kundelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ulinzi unaimarishwa mipakani ili kuzuia kuingiza vifungashio hivyo visivyokuwa na ubora.

Settings