​Mhandisi Malongo: Mradi wa Umeme Rufiji unazingatia mazingira

Oct, 01 2019

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema azma ya Serikali ya ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere iko pale pale na ujenzi wake unaendelea kwa kasi huku suala la hifadhi ya mazingira likizingatiwa.

Akizungumza na Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mazingira, Uhifadhi wa Maliasili na Usalama wa Nuklia kutoka Ujerumani Mhandisi Malongo amesema Tathmini ya Athari kwa Mazingira imefanyika na kuonyesha kuwa ujenzi huo ni salama kwa mazingira.

“Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mradi huu kwa kutumia fedha zake kutoka vyanzo vya ndani. Mradi huu utachukua eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 1,250 ambalo ni sawa na asilimia tatu (3%) tu ya eneo lote la pori la akiba selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000. Malongo alisisitiza.

Mhandisi Malongo amesema kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 81, mradi huu umefanyiwa tathimini ya athari kwa mazingira ili kubaini matokea hasi na chanya na kuweka mipango ya kudhibiti madhara na kuboresha utekelelezaji wake.

Amesema kuwa kiwango cha umeme cha megawati 2,100 kitaongezeka kwenye gridi ya Taifa kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na maendeleo ya viwanda na kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani, pamoja na uwepo wa fursa za kilimo cha umwagiliaji na uvuvi ulioboreshwa katika uwanda wa chini kutokana na usimamizi na udhibiti wa mtiririko wa maji.

Katika hatua nyingine Mhandisi Malongo amewafafanulia wabunge hao mafanikio yaliyopatikana katika katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini lililoanza kutekelezwa Juni Mosi na kusema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu kampeni hiyo imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa kwani imepokelewa kwa mtazamo chanya na wanachi ikiwa ni jitihada za kushirikisha taasisi mbalimbali na wadau kwa ujumla.

Akiongea kwa niaba ya wenzake kiongozi wa ujumbe huo Mhe. Sylvia Kotting-Uhl ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano na kuahidi ushirikiano na nchi yake katika kujenga uwezo katika nyanja za kusimamia na kudhibiti taka za kielektroniki, Uzalishaji wa Umeme wa jua na kutoa mwaliko kwa ujumbe wa Tanzania kutembelea Ujerumani kujifunza zaidi

Settings