Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito kwa wananchi kuangalia fursa zilizopo kwenye uwekezaji wa kurejeleza taka kwa lengo la kutunza Mazingira.
Akizungumza katika Ziara yake ya kikazi Kiwanda cha Chang You Plastic Recycling Industry Jijini Dar es salaam, Mhandisi Luhemeja alisema Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inahamasisha usafi na Utunzaji wa Mazingira.
“Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) tunahamasisha usafi na Utunzaji wa Mazingira, nitoe wito kwa wananchi kuangalia fursa zilizopo katika taka kama tunavyoona kwa sasa taka ni mali. Hivyo basi usafi wa Mazingira kupitia Urejelezaji wa taka ni fursa kwa vijana kujiajiri na kuongeza kipato“ alisema Mhandisi Luhemeja.
Pia Mhandisi Luhemeja amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kuhamasisha agenda ya urejelezaji wa taka kwa lengo la kuimarisha usafi wa Mazingira.
Kwa upande wake Mmiliki wa Kiwanda cha Chang You Plastics Recycling Industry ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za uwekezaji na fursa zilizopo ili kulinda Mazingira ambapo kupitia uwekezaji huo wa urejelezaji taka za plastiki kuwa bidhaa ameajiri zaidi ya wafanyakazi 80 kiwandani hapo.
Naye Mfanyakazi wa Kiwanda hicho Bi. Fasida Juma Issa alieleza kuwa kuwekeza katika taka kuna mafanikio makubwa kiuchumi kupitia urejelezaji wa taka hizo.