Makamu wa Rais azitaka sekta kuweka mikakati kukabili mabadiliko ya tabianchi

Oct, 19 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezitaka sekta zinazohusika na uhifadhi wa mazingira kujipanga upya na kuweka mikakati ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kikao kazi na viongozi mbalimbali wa serikali wanaohusika na sekta ya mazingira nchini, kikao kilichofanyika mkoani Dodoma. Amesema ni lazima kuweka utaratibu wa wadau wa mazingira pamoja na sekta zote muhimu husika kukutana mara kwa mara kwa lengo la ufuatiliaji wa maagizo na mipango uliyowekwa katika uhifadhi wa mazingira.

Makamu wa Rais ameagiza wakuu wa Mikoa nchini kuongeza jitihada za kuhakikisha usafi katika maeneo yao unafanyika kikamilifu. Amesema ni vema utaratibu wa kutumia siku za mwisho wa juma katika kufanya usafi wa pamoja kurudishwa ikiwemo katika maeneo ya barabara kuu ambayo yanakabiliwa na uchafuzi wa taka za plastiki kwa wingi. Aidha ameagiza kuwekwa kwa utaratibu maalum wa ufuatiliaji wa uhifadhi wa taka katika usafiri wa umma ili kudhibiti uchafuzi unaofanywa na watoa huduma hiyo ya usafiri katika maeneo mbalimbali.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia zoezi la kusafisha mitaro ikiwa ni njia ya kuimarisha usafi wa mazingira pamoja na kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za el nino zilizotabiriwa.

Pia Makamu wa Rais ameagiza kampeni za upandaji miti na usafi wa mazingira kuwa endelevu na kuhakikisha ufuatiliaji unafanyika wakati wote ili miti inayopandwa iweze kufikia lengo lililokusudiwa. Ameagiza zoezi la utoaji tuzo na motisha kwa wale wanaohifadhi vema mazingira kufanyika kikamilifu.

Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kuharakisha uzalishaji wa miche ya kutosha pamoja na kuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wa aina ya miche inayopaswa kupandwa kulingana na maeneo husika.

Makamu wa Rais amesisitiza elimu kwa wananchi kuendelea kutolewa kuhusu uhifadhi wa mazingira pamoja na kudhibiti uandaaji mashamba kwa kuchoma moto bila tahadhari hali inayopelekea athari kubwa kwa binadamu,viumbe hai na mazingira.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili usimamizi wa biashara ya kaboni, uhifadhi wa bonde la mzakwe mkoani Dodoma pamoja na vyanzo vingine vya maji, udhibiti wa mifugo inayoharibu mazingira pamoja na masuala ya nishati mbadala.

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi kutoka Wizara mbalimbali, wataalamu kutoka idara mbalimbali za serikali, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Viongozi wa Mkoa wa Dodoma pamoja na viongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami - Ruvu.

Settings