Makamu wa Rais awataka Wakuu wa Wilaya kuzingatia utawala bora

Mar, 13 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Wakuu wa Wilaya hapa nchini kuzingatia utawala bora, kanuni, sheria na utaratibu katika uongozi na utatuzi wa migogoro katika maeneo yao.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 13 Machi 2023 wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mtumba. Amesema ni vema viongozi hao kuzingatia maadili ikiwemo kudhibiti uvujaji wa siri za serikali kwa kujiepusha na matumizi yasiofaa ya mitandao ya kijamii pamoja na barua pepe binafsi katika kutuma nyaraka za serikali. Pia ametoa wito kwa Wakuu wa Wilaya kuzingatia utaratibu katika matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari katika ofisi za umma.

Aidha Makamu wa Rais amewataka Wakuu wa Wilaya kuwa wepesi na wabunifu katika kutatua migogoro hususan migogoro ya ardhi na mipaka, migogoro baina ya wakulima na wafugaji na baina ya wafugaji au wakulima na hifadhi na kuhakikisha hakuna migogoro mipya inayoibuka katika maeneo yao. Pia amewasihi kudhibiti uhasama ndani ya jamii au na vyombo vya dola, mauaji na kuwa walinzi wa haki za watu wote hususani wanawake na watoto.

Halikadhalika Dkt. Mpango amewataka Wakuu hao wa Wilaya kusimamia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango vilivyokusudiwa. Amewataka kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri, kudhibiti matumizi yasiyo na tija pamoja na kuziba mianya yote inayosababisha fedha nyingi za Serikali kupotea. Makamu wa Rais amewasihi Wakuu wa Wilaya kuhakikisha malipo mbalimbali katika maeneo yao yanafanyika kielektroniki na fedha zinapelekwa benki kwa wakati.

Makamu wa Rais amewasihi Wakuu wa Wilaya kuwa walinzi maadili, mila , desturi na utamaduni wa mtanzania kwa kutofumbia macho mmomonyoko wa maadili wa aina yeyote utakaojitokeza katika maeneo wanayosimamia. Amewataka kujiepusha na rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kutenda haki kwa wananchi na watumishi walio chini yao kuwahudumia wananchi kwa staha, kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Pia amesema ni muhimu kuongoza kwa mfano kwa kuwa makini wakati wote wanapozungumza na Umma kwa kuhakikisha wanatumia lugha fasaha na nzuri.

Vilevile Makamu wa Rais amewataka Wakuu wa Wilaya kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kutoa hamasa kwa wananchi hususani vijana ili wawe mstari wa mbele katika shughuli za uhifadhi ikiwemo kupanda miti na kusimamia mipango miji katika maeneo yao. Pia amewaasa kusimamia suala la uhifadhi wa vyanzo vya maji na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa.

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki amesema Wizara hiyo imelenga kuongeza jitihada katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi, kuweka mkazo katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, uendelezaji miji pamoja na kuhamasisha maendeleo vijijini.

Pia Waziri Kairuki amesihi Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanawahudumia vema wawekezaji na wenye nia ya kuwekeza hapa nchini kwa kuwa wafuatiliaji na kuondoa vikwazo kwenye masuala ya uwekezaji katika maeneo wanayosimamia.

Waziri wa Nchi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amewaasa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi, kutenda haki kwa watumishi wote, kuwa na mshikamano, kusimamia medani za siasa na utawala bora pamoja na kuwachukulia hatua watumishi wote wanaoenda kinyume na kanuni, sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Awali Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia kikamilifu suala la migogoro ya ardhi, na migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inasababishwa na viongozi katika maeneo husika kutotimiza wajibu wao kikamilifu.

Settings