Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Makamu wa Rais awataka wafanyabiashara wa gesi kuwasaidia wasiomudu gharama


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango amewataka wafanyabiashara hasa wa gesi ya kupikia majumbani kubuni mbinu za kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini ili waweze kumudu gharama za nishati hiyo mbadala.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Alisema pamoja na kuwepo kwa nishati mbadala ambazo watu huweza kuzitumia kama vyanzo vya kupikia lakini ukuaji wa matumizi wa nishati hizo ni wa asilimia mbili tu kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo Makamu wa Rais alibainisha kuwa tatizo kubwa lililopo ni namna gani unapunguza bei ya nishati mbadala na bei ya majiko hivyo aliviomba vyuo kufanya utafiti ni nini kinasababisha bei ya nishati mbadala na vifaa husika kuwa kubwa.

“Serikali, wadau wa maendeleo na asasi za kiraia na sekta binafsi hazina budi kuelekeza nguvu zaidi katika kutekeleza miradi inayolenga kuongeza matumizi ya nishati mbadala ya kupikia ikiwemo gesi, matumizi ya umeme wa jua, matumizi ya majiko banifu na vifaa vinavyotumia nishati kidogo katika kupika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine amezitaka Wizara, wakuu wa mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwahamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira na kufuatilia utekelezaji wake.

Alielekeza kila Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wapande miti milioni 1.5 kwa mwaka huku akizitaka Halmashauri na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuongeza jitihada za kusimamia mapori na kuzuia moto.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo alisema Kampeni Kabambe ya Utunzaji Mazingira inalenga kuhamasisha utunzaji na uhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema pia kampeni hiyo itasaidia kujenga uzalendo katika utunzaji mazingira na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano kwenye utunzaji mazingira duniani.