Makamu wa Rais awataka wadau wa madini kufuata sheria, kanuni

Jun, 20 2024

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wadau wote wa Sekta ya Madini kuzingatia na kufuata Sheria na Kanuni za madini ikiwa ni pamoja na kutotorosha madini ili kuondoa usumbufu na kurahisisha utendaji wa shughuli za wachimbaji na Serikali kwa manufaa ya wote

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wiki ya Madini linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema ni muhimu wachimbaji kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kulipa tozo na ushuru halali ili kusaidia kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Madini kwa kushirikiana vema na Wizara zinazohusika katika eneo la uchimbaji madini kwa ikiwemo Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Maji na Mazingira kabla ya kutoa leseni kwa wachimba madini ili kuepuka migogoro na muingiliano wa shughuli nyingine kulingana na matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo husika na kudhibiti uharibifu mazingira.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuongeza wigo na jitahada za utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia ili kuwaongoza vyema wachimbaji wadogo kutoka kwenye kuchimba kwa kubahatisha. Ameitaka Wizara hiyo kusimamia Sheria na Kanuni za uchimbaji bora na salama ili kuepuka ajali zisizo za lazima zinazopelekea vifo na majeraha kwa wachimbaji wadogo.

Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Madini kusimamia utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha kwamba madini yanayochimbwa yanaongezwa thamani nchini Tanzania na hivyo kusaidia kuongeza upatikanaji wa mapato na ajira kwa watanzania. Pia amesisitiza suala la kutowanyang’anya wachimbaji wadogo waliopata leseni za madini

kwa kigezo kuwa walipewa leseni hizo kwenye maeneo ya wachimbaji wakubwa.

Vilevile ameiagiza Wizara ya Madini na Tume ya Madini kuangalia uwezekano wa kuwataka wachimbaji wakubwa na wa kati wanaochimba madini yenye thamani kubwa kurejesha mchango wao kwa jamii katika maeneo yanayowazunguka.

Makamu wa Rais amewaasa wachimbaji wa madini kuwa na uchimbaji endelevu ambao unazingatia urejeshaji wa ardhi baada ya uchimbaji ili kulinda hifadhi ya mazingira ikiwemo uoto wa asili na vyanzo vya maji na kurejeza maeneo yaliyotumika kwa uchimbaji, katika hali yake ya asili na yaweze kutumika kwa shughuli nyingine za kiuchumi.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Wizara ya Madini katika bajeti ya mwaka 2024/2025 imetenga fedha nyingi katika kufanya tafiti za kina ili kuwaongoza vema wachimbaji madini katika shughuli zao. Ameongeza kwamba Wizara inatarajia kununua Helkopta mpya itakayofungwa vifaa maalum vya kuweza kufanya utafiti ili kufikia eneo kubwa la nchi.

Pia Waziri Mavunde amesema maabara kubwa na ya kisasa ya madini inatarajiwa kujengwa mkoani Dodoma ambayo itasaidia katika kutoa taarifa sahihi kwa wachimbaji madini nchini. Amesema sekta ya madini imeendelea kukua nchini ambapo imetoa mchango mkubwa kwa pato la taifa ikiwemo kuongezeka kwa makusanyo kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 725 kwa mwaka 2023/2024.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini nchini (FEMATA) John Bina amesema shirikisho hilo litaendelea kuwaunganisha wachimbaji wadogo na serikali ili kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji madini na ukuzaji wa uchumi. Pia amesema shirikisho hilo litatoa kipaumbele zaidi katika masoko ya madini ya viwandani na kuishauri serikali katika kuweka nguvu ya kutangaza madini ya Tanzanite.

Settings