Makamu wa Rais awaasa Watanzania kulea vyema watoto

Dec, 25 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma katika Ibada ya Sikukuu ya Krismasi leo tarehe 25 Desemba 2023. Ibada hiyo imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Emmanuel Mtambo.

Akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi kupitia kwa waumini hao, Makamu wa Rais amewasihi watanzania kusheherekea sikukuu kwa amani na utulivu pamoja na kujitoa kusaidia wale wasio na uwezo wakiwemo yatima.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania kuwalea vema watoto na kuwaongoza katika kumjua Mwenyezi Mungu, kuwafundisha uzalendo na kufanya kazi kwa bidii, kuwaongoza katika kuipenda nchi na kuitumikia wakiwa raia na baadae kuwa viongozi waadilifu.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa watanzania kuendelea kupinga aina zote za ukatili kwa wanawake na watoto. Amesema ni vema sikukuu ya Krismasi ikatumika kujitafakari na kuachana na tabia za kutupa watoto pamoja na utoaji wa mimba.

Vilevile Makamu wa Rais amewashihi waumini na viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa ili amani iweze kudumu na kuepushwa na mafarakano. Pia amewaasa watanzania kujiandaa ili kushiriki vema uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 pamoja na kuliombea taifa kupata viongozi waliobora.

Settings